📌 Tanzania yapongezwa kwa kuandaa Mkutano wa M300

📌 WB, AFDB kuunga mkono EAPP

📌Mawaziri wa Nishati Mashariki Mwa Afrika wakutana Uganda

Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Aprili 17, 2025 jijini Kampala nchini Uganda ameshiriki katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nishati wa nchi Wanachama wa Umoja wa Soko la Pamoja la Kuuziana Umeme katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (EAPP) na Mkutano wa Wakuu wa Mashirika au Taasisi za Umeme za nchi wanachama.

Kando ya mkutano huo, mawaziri hao walijadiliana kuhusu biashara ya kuuziana umeme miongoni mwa nchi wanachama.

Awali akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi wa Nishati wa Uganda, Mhe. Sidronius Opolot Akaasai amesema kuwa lengo la EAPP iliyoanzishwa Aprili 24, 2005 ni kuwa na uwiano sawa wa raslimali ya nishati katika ukanda huo.

Amesema hadi sasa EAPP ina nchi wanachama 13 na idadi inatarajiwa kuongezeka, ambapo nchi hizo zina nishati inayozalishwa kupitia vyanzo mbalimbali mfano maji, jua na gesi. Aidha, mahitaji ya umeme ni makubwa kuliko umeme unaozalishwa kwa sasa ambao ni megawati 19,000 pekee.

“Baadhi ya nchi bado zina changamoto ya nishati ya umeme na hivyo kushindwa kusambaza umeme kwa asilimia 100. Tunahitaji kuipa EAPP uwezo wa kutupatia umeme kwa vile nchi nyingi tayari zimeunganisha mifumo ya kusambaza umeme, sasa tunahitaji kufanya kazi pamoja ya kutimiza lengo letu la kuuziana umeme na kutumia vizuri raslimali tulizo nazo,” amesema Mhe. Akaasai.

Amebainisha kuwa kupitia mkutano huo, watazindua ofisi za Bodi Huru ya Udhibiti (Independent Reguratory Board- IRB) ya Ukanda wa Mashariki mwa Afrika wa Kuuziana Umeme ambayo tayari ina baadhi ya wafanyakazi ikiwa na lengo la kufanikisha masuala ya biashara ya kuuziana umeme kwa nchi wanachama.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Dkt. Kevin Kariuki ameipongeza Tanzania kupitia kwa Dkt. Biteko kwa kuandaa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika – Misheni 300 (M300) uliofanyika Januari 27-28, 2025 jijini Dar es salaam, kwa kuwa umeonesha dhamira ya dhati nchi ya kutumia raslimali zake kutatua changamoto ya nishati barani Afrika.

Naye, Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Dkt. Joseph Kapeka amesema WB itaendelea kuunga mkono jitihada za Marais wa Afrika kupitia M300 ambao unalenga kuongeza upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 300 Kusini mwa Jangwa la Sahara ifikapo mwaka 2030.

Mkutano huo wa EAPP umeanza Aprili 16 na kumalizika Aprili 17, 2025 ambapo ujumbe wa Tanzania umejumuisha Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesm Mramba pamoja na maafisa waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).