Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Kigoma
Baraza la Madiwani Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma limepitisha utiaji saini mkataba wa utekeleza, ujenzi, uendeshaji na usimamizi wa mradi wa Umwagiliaji Lumpungu wenye thamani ya zaidi ya sh. Bilioni 150 unaolenga kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao, uhakika na usalama wa chakula nchini.
Mradi huo, unatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Kibondo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), katika vijiji vya Kibuye, Kigina, Kisana,Nyarugusu, Kumshawabure, Kukinama,Magarama, na Nyaruhanga.

Akizungumza katika kikao maalumu cha baraza la madiwani na wadau wa maendeleo Mwenyekiti wa Halamshauri ya Kibondo, Habili Maseke, amesema kutokana na umuhimu wa mradi huo na mahitaji yaliyopo madiwani hao wamepitisha kwa kauli moja na wana kiu ya kuona mradi huo unatekelezwa kwa wakati.
Aidha lengo la mradi ni kukidhi mahitaji ya ndani na utoshelevu wa chakula, mahitaji ya malighafi kwa sekta ya viwanda vya kilimo na kuongeza mapato.
“Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuona kunakuwa na ushirikiano katika miradi kati ya Tume na Halmashauru, ombi langu ni kuona wakati wa utekelezaji wa mradi wananchi wazawa watoto wao wanapewa kipaumbele hata katika kazi ndogondogo,”amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, amesema mradi huo utatekelezwa ndani ya miezi 24 uliwa na thamani ya zaidi ya sh. Bilioni 150.
“Utahusisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, mabwawa mawili, nyumba, mashine ya kukubolea mazao na vifaa na zana za kilimo ambapo wakulima watakodi kwa bei nafuu ya serikali,”amesema.
Mndolwa amesisitiza kuwa, matarajio ya serikali ni kuona mradi huo unakwenda kubadili maisha ya wakulima ambapo watu binafsi na wakulima wadogo watashirikiana.
Amesema serikali imehakikisha inagawa hekta 2,000 za wakulima wadogo na hekta 5,000 kwa ajili ya wawekezaji wakubwa ambapo uwekezaji utakaofanyika utarudisha thamani ya mradi huo kwa serikali kuu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Agray Magwaza, amesema hatua hiyo iliyofikiwa na madiwani inaandika historia kwa maendeleo ya sekta ya kilimo wilayani humo na kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia katika kuufungua mkoa wa Kigoma Kiuchumi.
“Skimu hii inaenda kuleta matumaini kiuchumi, hatuna shaka na utekelezaji wa mradi huu hivyo tunaishukuru serikali kwa jinsi inavyohakikisha inapambania maendeleo ya mkoa huu,”amesema.










