Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku mikusanyiko ya wananchi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24, 2025, wakati Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, atakapofikishwa kwa ajili ya kesi ya uhaini inayomkabili.
Akizungumza Aprili 17, 2025 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, amesema jeshi hilo limebaini dalili za uwezekano wa kuvunjika kwa amani kutokana na mipango ya chama hicho kuhamasisha wananchi kufika mahakamani, hali inayotafsiriwa kama mbinu ya kushinikiza vyombo vya sheria.
Muliro amesisitiza kuwa jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo, akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja dhidi ya watakaokiuka.
Marufuku hiyo inakuja baada ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, kuhamasisha wanachama na wananchi kufika kwa wingi mahakamani siku hiyo, wakiwa na vitambaa vyeupe na maji kama alama ya kudai haki kwa amani bila silaha wala vurugu.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Aprili 16, 2025, katika viwanja vya Mbezi, Wilaya ya Ubungo, Heche alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi kwa njia ya amani, lakini Jeshi la Polisi limeweka msimamo wake wazi halitavumilia mkusanyiko wowote.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linatambua kuwa kuanzia Aprili 18, 2025 waumini wa dini ya Kikristo wanaanza kuungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Pasaka itakayosherehekewa tarehe 20.4.2025. Sikukuu hiyo huhusisha ibada mbalimbali ambazo hufanyika katika nyumba za ibada mchana na usiku.
Hivyo Polisi Dar es Salaam imejipanga vizuri kuhakikisha waumini wanashiriki na kusherehekea Sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.
Wito unaendelea kutolewa kwa wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wakati wa matembezi na mikusanyiko mbalimbali, pia nyumba na makazi
yasiaachwe bila uangalizi wakati wa sherehe hizi.
Pia Suala la Usalama barabarani imesisitizwa kwa madereva wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria ili kuepusha ajali zisizokuwa na ulazima.
