*Amwambia chama, Rais Samia wanaamini katika maridhiano, kutii sheria

*Asisitiza CCM haina visasi wala chuki na yeyote

*Amwambia Lissu anatuhumiwa kuikosea Jamhuri sio CCM, hivyo watamalizana mahakamani

Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amewahakikishia Watanzania kwamba Chama hakina chuki wala kısası na mtu yeyote na kinaamini katika sera ya maridhiano.

Pia, amesema kuwa menyekiti au makamu mwenyekiti wa chama cha siasa haikupi uhalali wa kuwa juu ya sheria, hivyo iwapo utafanya kosa lolote Jeshi la Polisi litakukamata na sheria itachukua mkondo wake bila kujali nafasi uliyonayo.

Wasira alitoa kauli hiyo jana akiwa katika mkutano wa hadhara alipokuwa akizungumza na wana CCM na wananchi wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora ambako anaendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani, kuzungumza na viongozi wa CCM na kusikiliza kero za wananchi.

Akiwa katika huo mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Shaban Warioba alitumia muda wa maswali na majibu kumuombea msamaha Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu ambaye kwa sasa anaishikiliwa na vyombo vya dola na kwamba kama ana makosa CCM na serikali imsamehe, imuachie huru kwa kuwa hakuna binadamu aliyekamilika.

Akimjibu mfuasi huyo mbele ya mamia ya wananchi, Wasira alisema CCM inaamini katika maridhiano na kwamba maridhiano ni sera ya Chama na na serikali chinibya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ndio maana hata Tundu Lissu alipokuwa amekimbia nchi maridhiano ndiyo yalimrudisha nchini.

“Yule bwana mwenye kuuliza na wengine mliokuwa mnamsikiliza niwasaidie tu kuwaelimisha kwamba mkiwa na sera ya maridhiano haiwi mbadala wa sheria na wala huwezi kusema kwa sababu wewe ni mwenyekiti basi upo juu ya sheria.

“Wote tuko chini ya sheria hata mimi nikiamka sasa hivi nikakupiga kofi Jeshi la Polisi watanikamata hawawezi kusema wewe ni Makamu Mwenyekiti wa CCM maana umakamu haunipi uhuru wa kupiga watu makofi halafu nikaondoka salama.

“Kwa hiyo na ninyi na chama chenu CHADEMA tunakiheshimu sana lakini unatwambia kwamba CCM tumsamehe, sisi hajatukosea ameikosea Jamhuri na ndiyo inaye, hivyo tuiachie Jamhuri maana hatuwezi kuingilia mahakama. Kama ikiona hakuna hoja itamwachia kama ambavyo inakamata watu wengine na kukiwa hakuna kosa inawaachia,” alisema.

Akifafanua zaidi kumjibu mfuasi huyo wa CHADEMA, Wasira alisisitiza CCM haina visasi na mtu, lakini atakayekosea hukamatwa na polisi kwa kuwa polisi wamesomeshwa kukamata, vilevile wamesomeshwa kusema kosa hili ni kosa, “sio kila anayekamatwa huwa polisi wametumwa, sio kweli.”

“Umekuja kuuliza swali ukiamini sisi ni chama cha maridhiano na wewe unataka uridhiane na sisi tunakubali una hoja yako, labda tuwaachie wenye kushtaki waelewane kule mahakamani halafu mambo yao yakiisha sisi tutakaa naye na tunazungumza.

“Hata Aprili 2 (mwaka huu) mwaka huu mini nilikuwa na mkutano na yeye (Tundu Lissu) kabla hayo mnayoyasema (kukamatwa) hayajatokea na yeye ndiye alikuwa mwenyekiti wa mkutano niliokuwepo, na mimi nilikubali kuwa chini ya uenyekiti wake na tukakubaliana yale tuliyokubaliana yachakatwe na makatibu wakuu wa vyama.

“Halafu baadae tukae tena Aprili 14, lakini kwa bahati mbaya chama chako hakikuja, kama hakikuja tutajua kinafikiri nini? Lakini sisi hatuna visasi kwa sabaabu huu ni mfumo wa vyama vingi na vyama vyote vya siasa vina haki, lakini vina haki kwa kufuata sheria

Awali Shabani Swae Mushio Warioba alitoa ombi kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Wasira akidai amemsikia Mwenyekiti wa chama chake cha CHADEMA yuko ndani, hivyo anataka kujua amefanya kosa gani na kama amefanya kosa anaiomba serikali ya Chama Cha Mapinduzi imsamehe hata kama ana makosa.