China imegeukia uagizaji wa mafuta kutoka Canada baada ya kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka Marekani kwa karibu asilimia 90 huku vita vya kibiashara vikiendelea.
Upanuzi wa bomba la mafuta Magharibi mwa Canada ambao ulifanyika chini ya mwaka mmoja uliopita umeanza kunufaisha China na waagizaji wengine wa mafuta wa Asia Mashariki kutokana na upanuzi wa upatikanaji wa akiba kubwa ya mafuta ambayo hayajasafishwa eneo la Alberta
Uagizaji wa mafuta wa China kutoka bandari yenye bomba karibu na Vancouver uliongezeka hadi mapipa milioni 7.3 kwa mwezi huu wa Machi ambayo haijawahi kutokea, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa viwango hivyo kuongezeka, kulingana na takwimu kutoka Vortexa Ltd.
Wakati huo huo, uagizaji wa mafuta kutoka Marekani umepungua hadi mapipa milioni 3 kwa mwezi kutoka kilele cha mapipa milioni 29 mnamo mwezi Juni.
Mabadiliko hayo ni mfano mwingine wa msukosuko wa kiuchumi na kimkakati uliosababishwa na hatua zilizochukuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump za badilisha uhusiano wa kibiashara kimataifa.
