Boti ya mbao iliyokuwa na abiria wapatao 400 ilishika moto na kupinduka karibu na mji wa Mbandaka.

Ajali hiyo ilitokea Kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenye Mto Congo, na kuwaacha watu wasiopungua 50 wakiwa wamekufa na wengine hawajulikani walipo.

Kamishna wa Mto Congo Loyoko, aliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba ajali hiyo ilitokea mtu mmoja alipokuwa akipika kwenye boti.

Hatahivyo, abiria kadhaa, pamoja na wanawake na watoto, walikufa baada ya kuruka ndani ya maji bila kuwa na uwezo wa kuogelea.

Takriban waathirika 100 walipelekwa kwenye makazi ya muda katika ukumbi wa mji wa Mbandaka, wengi wao wakiwa na majeraha mabaya ya moto.

Desemba mwaka jana,watu wasiopungua 38 walikufa baada ya kivuko kilichobeba zaidi ya watu 400 wanaosafiri kwa ajili ya Krismasi kupinduka kwenye mto kaskazini mashariki mwa DRC.