Na Mwandishi Wetu, Kibiti
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bungu, Mhe. Ramadhan Mpendu, ameongoza zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Nyambili–Nyambunda jana, ikiwa ni sehemu ya kampeni endelevu ya kutunza mazingira.
Katika zoezi hilo, jumla ya miti 150 ya matunda na kivuli imepandwa shuleni hapo, ambapo Mhe. Mpendu aliipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa uzalishaji na usambazaji wa miche bure kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
“Tutunze miti, itatufaa kwa vizazi vijavyo. TFS wamefanya kazi kubwa – miche hii ni dira ya mustakabali wa mazingira bora,” alisema Mhe. Mpendu mara baada ya zoezi hilo kukamilika.

Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Omari Msumi, Mkuu wa shule ya Sekondari Nyambili–Nyambunda, walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo ambao walishiriki kikamilifu katika upandaji miti.
Mhe. Mpendu pia aliwatia moyo walimu na wanafunzi kwa kujitoa kwao katika kutunza mazingira, akisema shule hiyo inatoa mfano bora wa kuigwa katika kulinda rasilimali za asili.

