Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesifu kupevuka kwa maono ya kisiasa yalioonyeshwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu ,aliyeitangazia dunia chama chake kitashiriki uchaguzi Mkuu oktoba mwaka huu bila longolongo.
Pia CCM kimebaini kuwepo tofauti ya uelewa, upeo, busara na ufahamu kati ya Kiongozi wa ACT na Mwenyekiti wake Othman Masoud Othman .
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi , Uenezi na Mafunzo ,Khamis Mbeto Khamis, aliyesema kwa chama makini ni aibu kukimbia uchaguzi wa kidemokrasia.
Mbeto alisema haki ya kushiriki uchaguzi inawahusu zaidi wananchi kupitia vyama vyao lakini si halali kwa viongozi wa Vyama vya siasa kuwazuia wananchi wasitumie haki na wajibu wa kuchagua au kuchaguliwa.

Alisema si hivyo tu ,bali kiongozi wa ACT Wazalendo amezungumza mambo ua msingi akitumia lugha komavu ,maneno yenye hekima na busara, tofauti na matamshi holela yanayokuwa yakitolewa mara kwa mara na Mwenyekiti wake.
“Viongozi wa Vyama vya Siasa wasipore madaraka na haki za wananchi Waache kuwazuia ili wasishiriki chaguzi za kidemokrasia. Haki za vyama zisikwapue matakwa ya kisheria na kikatiba ya wananchi na kugeuza miliki ya viongozi wa vyama ” Alisema Mbeto
Aidha Katibu huyo Mwenezi alisema maelezo alioyatoa kiongozi wa ACT Wazalendo, hayakuambatana kabisa na maneno ya vitisho au yenye kujenga hofu na taharuki katika jamii .
“Kiongozi wa ACT amejenga hoja zake bila kutumia lugha ya ubabe tofauti na Mwenyekiti wake .Hii ni tofauti iliopo kati ya Mwenyekiti na kiongozi wa chama. Ama kweli maarifa ya kinamama huwazidi baadhi ya kinababa ‘ Alieleza
Hata hivyo, katika maelezo yake, Mbeto akimtaka Semu afute ndoto za ACT kukishikda CCM kwakuwa hakijapata uwezo huo na wananchi hawajawa tayari kukiamini ACT ili kuiongoza Zanzibar.
Pia Mbeto alisema chini ya usimamizi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Tume huru ya Uchaguzi Tanzania, vyama vya upinzani vimekuwa vikishinda na kupata viti vingi ikiwemo kura za urais .
“Ni masikitiko kwa ACT Wazalendo kumsimamisha Othman kuwania nafasi ya urais ili ashindane na mgombea wa CCM Rais Dk Huseein Ali Mwinyi. Tunakwenda kushinda mapema asubuhi kweupe” Alisema Mbeto
Katibu huyo Mwenezi alisema kulingana na kazi kubwa ilofanywa na Serikali ya awamu ya nane, CCM kina kazi nyepesi mno ifikapo oktoba mwaka huu.