Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameongoza harambee maalum ya wadau wa elimu nchini kuchangia Kongamano la eLearning Africa, ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 1.6 zimepatikana.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Saalaam kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, Ulega amesema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la kimataifa, ambalo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Aliongeza kuwa, “matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ni lazima katika mifumo ya utoaji elimu,” alisema Ulega. SOMA : TAMISEMI: Kuna mageuzi makubwa sekta ya elimu.
Aidha, Waziri Ulega alieleza kwamba hatua hii inatokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameimarisha diplomasia ya kimataifa na kuleta manufaa katika sekta mbalimbali, ikiwemo utalii na elimu. “Hatuna budi kuendelea na mabadiliko katika elimu zetu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukuza teknolojia katika elimu, na kwamba kongamano hilo litaona ushiriki wa zaidi ya wadau 1,500, wakiwemo Mawaziri wa Elimu kutoka nchi 50 zaidi. Alitoa wito kwa vijana na wabunifu kujisajili ili kushiriki katika maonesho na mijadala itakayofanyika.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, aliongeza kuwa tukio hili ni uthibitisho wa uwezo wa nchi katika kuandaa mikutano ya kimataifa na kuonyesha dhamira ya serikali ya kuwekeza katika elimu na teknolojia. “Tunatarajia matokeo chanya yatakayochochea maendeleo ya elimu nchini,” alisema Prof. Nombo.
