Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani ilisema Chuo Kikuu cha Harvard kitapoteza uwezo wa kusajili wanafunzi wa kigeni ikiwa haitakubali kutimiza matakwa ya serikali ya Trump kushirikisha taarifa za baadhi ya wamiliki wa visa, kuashiria kuongezeka kwa mtafaruku kati ya serikali na taasisi hiyo ya elimu.
Waziri wa Wizara ya Usalama wa Ndani Kristi Noem pia alitangaza siku ya Jumatano kusitishwa kwa ruzuku mbili kwa chuo hicho cha Harvard.
Noem alisema aliandika barua kwa Harvard akidai rekodi ya kile alichokiita “shughuli haramu na za dhuluma” zinazofanywa na wanafunzi raia wa kigeni wa Harvard ifikapo Aprili 30.
“Na ikiwa Harvard haiwezi kuhakikisha kuwa inafuata kabisa mahitaji yake ya kuingia katika chuo hicho, kitapoteza fursa ya kusajili wanafunzi raia wa kigeni,” Noem alisema katika taarifa.
Msemaji wa Harvard alisema chuo kikuu kinafahamu kuhusu barua ya Noem “juu ya kufutwa kwa ruzuku na uchunguzi wa visa za wanafunzi wa kigeni.”
Utawala wa Rais Donald Trump umetishia vyuo vikuu na kupunguza ufadhili wa serikali kutokana na maandamano ya vyuo ya Palestina dhidi ya wanajeshi wa mshirika wa Marekani Israel huko Gaza baada ya shambulio la Oktoba 2023 na wanamgambo wa Hamas wa Palestina.
Utawala wa Trump pia unajaribu kuwafukuza waandamanaji wengine wa kigeni na kuwapokonya mamia ya visa kote nchini humo.
