Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini kuwa mashirika kadhaa ya umma yamesaini mikataba yenye thamani kubwa bila kufuata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wala maafisa wa sheria wa ndani.
Mikataba hiyo, yenye jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 58.03, dola milioni 1.23 za Marekani (Sh bilioni 3.30), na Yuro milioni 4.20 (Sh bilioni 12.76), ilitiwa saini bila kufanyika kwa uhakiki wa kina kuhusu umahiri na uwezo wa wakandarasi au wasambazaji.
Ripoti ya CAG inaonesha kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilikiuka ushauri wa kufanya tathmini ya kina baada ya zabuni, kwa kutegemea tu historia ya zamani ya wazabuni wake. Vivyo hivyo, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ilipuuzia ushauri wa kufanya uchambuzi wa hali ya kifedha, kisheria na kiutendaji wa mshauri aliyehusika katika mkataba wa Yuro milioni 4.20.
Shirika la Reli Tanzania (TRC) nalo lilisaini mikataba ya Sh milioni 257 licha ya maoni ya kisheria kuonyesha kasoro kwenye tarehe za uwasilishaji wa bidhaa. Bidhaa zilicheleweshwa kufikishwa, hali inayothibitisha athari za kupuuza ushauri wa kisheria. Vilevile, Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Dodoma lilisaini mikataba ya Sh milioni 788 bila uhakiki sahihi, kinyume na kanuni.
Hata hivyo, ripoti hiyo inatoa nuru kwa kupungua kwa idadi ya mashirika yasiyofanya uhakiki wa kina: kutoka mashirika 8 mwaka 2021/22 hadi shirika moja tu mwaka 2023/24. “Kusaini mikataba bila kutathmini uwezo wa wasambazaji kunaweza kuathiri utekelezaji wa miradi na kuongeza hatari za kisheria,” imeeleza ripoti ya CAG.
CAG amependekeza mashirika yote ya umma kuhakikisha michakato ya tathmini inafanyika kikamilifu kabla ya kusaini mikataba. Aidha, ushauri wa kisheria uzingatiwe ili kuepuka masharti mabaya na kulinda maslahi ya taifa.
