Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Pwani
Wanachama wa vyama vya ushirika nchini wametakiwa kutokuwa waoga kuwabainisha viongozi wabadhilifu ili kusaidia kuleta uhai na ustawi wa vyama vya ushirika.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, Tito Haule, alitoa rai hiyo wakati wa Jukwaa la Tano la Maendeleo ya Ushirika lililofanyika April 16,2025 katika ukumbi wa Destiny Hall, Kibaha kwa Mathias, mkoani Pwani.
“Tusiogope kuwataja wale wanaofanya ubadhilifu katika vyama vyetu, kuwafichua ni hatua ya kulinda rasilimali zetu na kuhakikisha vyama vinaendeshwa kwa uwazi na uadilifu,” alieleza Haule.

Vilevile Haule alisisitiza umuhimu wa viongozi kuzingatia uwajibikaji, ushirikishwaji, uadilifu na ubunifu kama nguzo kuu za kuimarisha vyama vya ushirika ili kuvutia wengine kujiunga.
Aidha, aliwataka maofisa ushirika na wadau wengine kuhakikisha wanazingatia sheria katika kusimamia shughuli za vyama, huku akipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya ushirika.
“Serikali imetoa kiasi cha sh. Bilioni 5 kama mtaji kwa ajili ya kuimarisha Benki ya Ushirika ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni” Na kuboresha mifumo ya TEHAMA na upatikanaji wa pembejeo, hatua ambayo imeongeza tija katika kilimo,”
Shangwe Twamala, Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alihimiza mshikamano miongoni mwa wanachama, akisema
“Ili vyama viwe imara, lazima tushirikiane na kushirikishana katika kila hatua.”

Nae Abdillah Mutabazi, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, alieleza kuwa Mkoa wa Pwani una vyama vya ushirika 202, ambapo 159 vimesajiliwa rasmi.
Kwa mujibu wa Mutabazi, msimu wa 2024/2025, vyama vya msingi vya kilimo (AMCOS) ,minada minne ilifanyika na kufanikisha mauzo ya kilo 21,622,919 zenye thamani ya sh. 67,004,410,900.65, na ufuta, minada sita ilifanyika na kuuza kilo 13,083,808.5 zenye thamani ya Shilingi 48,112,587,948.06.