Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato
ZAIDI ya shilingi milioni 431.2 zimetumika kwaajili ya kutekeleza mradi wa uchimbaji visima vitano kwenye vijiji vilivyokuwa na ukosefu mkubwa wa maji safi na salama kwenye Jimbo la Chato mkoani Geita.
Huo ni mpango mkakati wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imetoa fedha kwaajili ya kuchimba visima 900 nchi zima ili kunusuru maisha ya wananchi wa vijijini ambao walikuwa hawajafikiwa kabisa na huduma za maji ya bomba.

Meneja wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani Chato,Avitus Exavery, amesema hayo mbele ya mkuu wa wilaya hiyo ambaye alikuwa katika ukaguzi wa miradi ya maji vijijini na kusikiliza kero mbalimbali.
Amevitaja vijiji vilivyo nufaika na mpango huo katika Jimbo la Chato kuwa ni Ludeba,Nampalahala, Nyantimba,Malebe na Kibumba.
Amesema miradi hiyo inakusudia kuwanufaisha wananchi zaidi ya 33,745 waliopo katika maeneo ya vijijini kwenye Jimbo hilo na kwamba hadi kufikia Mei 30,2025 upatikanaji wa maji kwenye vijiji hivyo utakuwa aslimia 60.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Kibumba,Clement Guri,mbali na kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa ya kuondoa adha kwa wananchi wa vijijini amesema huduma hiyo ni muhimu sana kwa wakazi wa eneo lake kutokana na vyanzo vingi vya maji kuchafuliwa na shughuli za uchimbaji madini.

“Mradi huu kwetu ni mkombozi mkubwa kwa maana maji yaliyokuwa yakitumiwa na wananchi awali kwaajili ya kunywa,kunawa,kupikia,kuoga na matumizi mengine yalikuwa yakichafuliwa na shughuli za uchenjuaji Madini” amesema Guri.
Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti jimboni humo,Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Peter Bura, amewataka wananchi kutambua uwekezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo unaoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita kwa manufaa mapana ya Umma.

Aidha amezitaka kamati za usimamizi na utumiaji maji vijijini kufanya vikao vya mara kwa mara,kusoma mapato na matumizi pamoja na kuvitunza vyanzo vya maji kwa mujibu wa sheria za nchi.
Vilevile amesema wilaya ya Chato haina budi kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa za serikali kwa kuilinda miundombinu iliyopo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo hatua itakayo saidia kutelekezwa kwa miradi mingine ya kimaendeleo.
“Ninaamini wananchi wa Chato hakuna tunachomdai mama Samia kutokana na miradi mingi ya maendeleo aliyotuletea, ispokuwa yeye ndiye anayetudai, na kama mnavyojua muungwana siku zote huwa anapopewa anashukuru” amesema Bura.
