Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ameiagiza Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushughulikia changamoto ya ukuaji wa haraka wa miji (urbanization) ili kuwe na mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Waziri Masauni aliyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akizundua bodi ya tisa ya NEMC itakayoongozwa na Mkuu wa Mkoa mstaafu, Mhandisi Mwanasha Tumbo.

Alisema miji inakua kwa kasi bila mipango bora ya matumizi ya ardhi hali inayosababisha msongamano, uchafuzi wa mazingira, ukosefu wa mifumo ya maji safi na taka na uharibifu wa vyanzo vya maji na kingo za mito na bahari.
Pia Waziri Masauni aliagiza bodi hiyo kufanya vikao vyake kama mujibu wa sheria na iweke mikakati madhubuti ya kupata fedha za kujiendesha.
“Nawaagiza mshirikiane kwa karibu na menejimenti ya Baraza ili kuleta matokeo yenye tija na msimamie vizuri Baraza ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira nchini,” alisema.
Aidha, Waziri aliwataka wahamasishe elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwani wananchi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Alisema kwa wananchi kukosa elimu ya mazingira kumechangia washiriki katika shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira kama ukataji miti hovyo, uchomaji misitu na utupaji taka ovyo.
“Hakikisheni Baraza linakuwa mamlaka ya usimamizi wa mazingira nchini na linakabiliana ipasavyo na mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa joto duniani, kupungua kwa mvua au mvua zisizotabirika, na majanga kama mafuriko au ukame vinachangia kuharibu mazingira na rasilimali za asili,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi alisema baraza hilo limekuwa likifanya uchunguzi utakaosaidia usimamizi na uhifadhi wa mazingira unaofaa na kuratibu utafiti na uchunguzi kwenye mazingira ili kukusanya na kusambaza taarifa kuhusu matokeo ya utafiti na uchunguzi huo.
Alisema NEMC imekuwa ikipitia taarifa ya tathmini ya athari za mazingira na kupendekeza kuhusu utoaji wa idhini ya taarifa za athari kwa mazingira kwa kampuni zinazotekeleza miradi mbalimbali.
Alisema NEMC imekuwa ikibainisha aina ya miradi na programu zinazotakiwa kufanyiwa uhakiki wa mazingira au upelembaji wa mazingira chini ya Sheria ya EIA na kusimamia udhibiti na utekelezaji wa viwango vya ubora wa mazingira kitaifa.

“NEMC imekuwa ikianzisha na kubuni taratibu na kinga za kuzuia ajali zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira na pia kubuni hatua za marekebisho pindi zitokeapo ajali pamoja na kuanzisha programu zinazokusudia kuendeleza elimu ya mazingira na elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa usimamizi mwafaka wa mazingira,” alisema
Alisema wamekuwa wakichapisha na kusambaza vitabu vya miongozo, kanuni za kisheria au miongozo kuhusu usimamizi wa mazingira na kuzuia au kupunguza uharibifu wa mazingira.
Alisema NEMC imekuwa ikitoa ushauri wa kitaalamu kwa vyombo vinavyojihusisha na usimamizi wa maliasili na mazingira ili kuviwezeshesha kutekeleza wajibu wake na kutekeleza kazi nyinginezo zinazotolewa na Waziri anayehusika na mazingira.
