Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa anaamini Iran inachelewesha kwa makusudi kufikiwa kwa makubaliano ya nyuklia, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kuigharimu nchi hiyo kwa kiasi kikubwa, ikiwemo uwezekano wa kushambuliwa kijeshi.
Akizungumza na waandishi wa habari nchini Oman siku mbili baada ya mazungumzo kati ya Tehran na Washington, Trump alisema, “Nadhani wanatufanyia mchezo.”
Alisisitiza kuwa Iran iko katika hatua za mwisho kuelekea kutengeneza silaha ya nyuklia na akaitaka Tehran kuchukua hatua za haraka ili kuepuka kile alichokiita “adhabu kali.”
Kwa muda mrefu, Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani pekee, ikikanusha madai kuwa inalenga kutengeneza silaha za nyuklia.
Wakati mazungumzo ya pili kati ya Marekani na Iran yakitarajiwa kufanyika hivi karibuni, taarifa zinazokinzana zimeibuka kuhusu mahali patakapofanyika vikao hivyo muhimu vya kidiplomasia.
Katika hatua nyingine, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha vikwazo dhidi ya raia saba wa Iran na taasisi mbili, kufuatia kile walichokielezea kuwa ni vitendo vya kuwazuilia raia wa Umoja wa Ulaya nchini Iran kinyume cha sheria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, alisema alipowasili Luxembourg kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya: “Ninafarijika kwamba leo tumeweza kupitisha vikwazo hivi, ambavyo vinahusisha pia Gereza la Shiraz.
”Ilikuwa ni hatua ya lazima kuchukuliwa, kwa kuwa mazingira ambayo raia wetu, Wafaransa na Wazungu, wanazuiliwa ndani ya Iran hayawezi kuvumilika.”
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, orodha ya waliowekewa vikwazo inajumuisha mkuu wa Gereza la Evin, majaji kadhaa, pamoja na maafisa wengine wa idara ya mahakama ya Iran.
Vikwazo hivyo vinahusisha kufungiwa mali walizonazo ndani ya mataifa ya EU na marufuku ya kusafiri kwenda nchi hizo.
Umoja wa Ulaya umetaja vitendo hivyo vya Iran kama “utekaji nyara wa kimataifa unaofadhiliwa na serikali.” Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la shughuli za kidiplomasia kuhusiana na suala la nyuklia la Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, anatarajiwa kusafiri kwenda Moscow wiki hii kwa mashauriano ya kidiplomasia.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, anatarajiwa kufanya ziara ya Tehran kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pamoja na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la nchi hiyo.
