Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Bodi ya Maziwa nchini imeweka wazi mpango wake wa kuanzisha Bar maalum za maziwa (Maduka)katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwa ni juhudi za kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa njia endelevu na kuvutia zaidi.
Mpango huo unalenga kuboresha Afya kwa wanatanzania na kuwa chachu katika kufungua milango kwa wafugaji kuuza maziwa yao kwa uhakika wa soko, jambo litakaloongeza kipato chao na kuinua uchumi wa maeneo ya Mjini na vijijini.
Hayo yameelezwa leo Aprili 15 ,2025 Jijini Dodoma na Msajili wa bodi ya maziwa Tanzania (TDB)Prof.George Msalya kwenye kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo na kueleza kuwa iwapo itafanikiwa utasaidia kuinua afya ya wananchi pamoja na kukuza soko la maziwa kwa wakulima wa ndani.

Akizungumza katika kikao hicho,Msajili huyo amesema kuwa Bar hizo zitakuwa ni sehemu maalum ambapo wananchi watapata fursa ya kufurahia bidhaa za maziwa zenye ubora wa hali ya juu zikiwemo aina mbalimbali za maziwa safi, mtindi na bidhaa nyingine zitokanazo na maziwa.
sisitiza kuwa mradi huo utaanza kwa majaribio katika mikoa kadhaa kabla ya kusambaa nchi nzima na kuongeza ajira kwa vijana, hasa wale watakaoajiriwa kama wahudumu, wauzaji, na wasambazaji wa maziwa.
“Tunataka kuondoa ile dhana kuwa maziwa ni kwa ajili ya watoto au wagonjwa pekee,kupitia bar hizi, tutahamasisha unywaji wa maziwa kama sehemu ya maisha ya kila siku kwa watu wa rika zote,” amesema
Ameongeza kuwa bar hizo zitakuwa na mazingira rafiki na ya kuvutia, yenye huduma bora na wafanyakazi waliopatiwa mafunzo mahsusi kuhusu Afya na mazingira.
Bodi hiyo pia imeweka mkazo katika usalama wa chakula na ubora wa bidhaa zitakazotolewa katika bar hizo ambapo kwa kushirikiana na mamlaka za afya na viwango, watasimamia kwa karibu kuhakikisha kila bidhaa inayotolewa inakidhi vigezo vya kiafya na viwango vya kitaifa.
“Usalama wa mlaji ni jambo la kipaumbele kwetu,elimu kwa umma kuhusu faida za kiafya za unywaji wa maziwa itaambatana na uzinduzi wa bar hizoKampeni za mitandaoni, redio na televisheni zitazinduliwa ili kuhakikisha jamii inapata uelewa mpana kuhusu umuhimu wa lishe bora inayojumuisha maziwa. Meneja huyo aliitaka jamii kuunga mkono mpango huo kwa moyo wa uzalendo na afya njema.

Kwa sasa, bodi imeanza kushirikiana na halmashauri za mikoa pamoja na sekta binafsi ili kuweka mikakati ya utekelezaji wa haraka. Taarifa zaidi kuhusu ratiba ya uzinduzi wa bar za maziwa zinatarajiwa kutolewa katika wiki zijazo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Charles Mhina ametumia kikao hicho kutoa wito kwa watumishi hao wa TDB kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kujituma huku akisisitiza kuwa maadili hayo ndiyo msingi wa uwajibikaji na utekelezaji bora wa majukumu ya kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe , Dkt. Mhina amesema mafanikio ya bodi hiyo yanategemea zaidi nidhamu ya ndani na utendaji uliotukuka wa watumishi wake.
Amewaasa watumishi kuzingatia maadili ya kazi kwa kuonesha uwazi, uwajibikaji na kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza mipango ya taasisi hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa bodi hiyo ina jukumu kubwa la kukuza sekta ya maziwa nchini.
“Hatutaweza kufanikisha dhamira ya kuendeleza sekta hii muhimu kama hatutakuwa na nidhamu ya kazi na moyo wa uzalendo,” amesema Mkurugenzi huyo.
Amesisitiza umuhimu wa kila mtumishi kutimiza wajibu wake kwa wakati na kwa ufanisi ili kuiwezesha bodi kufikia malengo yake ya kimkakati na kwamba uwajibikaji wa mtumishi mmoja mmoja utasaidia kuongeza tija na kuleta mabadiliko chanya katika utendaji wa jumla .
“Kwa kuwa Bodi iko katika hatua muhimu ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo uhamasishaji wa unywaji wa maziwa na kuimarisha soko la maziwa kwa wakulima na wafugaji nawahimiza kila mtumishi kutambua nafasi yake na kutoa mchango wa dhati katika kufanikisha malengo ya kitaifa,”amesema.
Mkurugenzi huyo pia amewataka watumishi kuwa tayari kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya kisekta na kiteknolojia na kueleza Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuhakikisha wana ujuzi na maarifa ya kisasa yanayohitajika katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sekta ya maziwa, “ameeleza