Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Nairobi
Wiki iliyopita sikuandika katika safu hii. Sikuandika si kwa sababu nyingine bali hekaheka za uchaguzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambapo nawashukuru wanachama wa TEF kwa heshima kubwa waliyonipa ya kunichangua kwa kishindo bila kupingwa. Katika uchaguzi huu uliofanyika katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, makamu wangu Bakari Machumu naye pia amepita bila kupingwa. Bila shaka hii ni imani kubwa mliyoonyesha kwetu ninyi wahariri, hivyo na sisi hatutawaangusha.
Nawapongeza wajumbe saba waliochanguliwa pia, Joseph Kulangwa, Salim Said Salim, Bakari Kimwanga, Stella Aron, Caren Tausi Mbowe, Anna Mwasyoke na Jane Mihanji. Najivunia safu hii, ambayo idadi ya wanawake imeongezeka zamu hii katika uongozi wa TEF. Uchaguzi huu ulikuwa moto wa kuotea mbali. Tulitikisana, walioshinda ni kicheko na walioshindwa walijifariji kwa K-Vant safari yote ya Songea – Dar es Salaam.
Sitanii, wiki iliyopita ilikuwa ya burudani ya kipekee kwa upande mmoja na machungu kwa upande mwingine. Tumeshuhudia timu kubwa ya Simba Sports Club ikiisasambua Klabu ya Al Masry inayoshikilia nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ya Misri. Simba sasa inacheza nusu fainali ya Kombe la Washindi barani Afrika, baada ya mara ya mwisho kufikia hatua hii miaka 32 iliyopita, yaani mwaka 1993. Hongereni wanasimba, hongereni Watanzania kwani ushindi huu ni wa nchi yetu na unalitangaza taifa letu kuliko utani wetu wa “vyura” na “makolo”. Ila naomba Uwanja wa Mkapa ukarabatiwe. Umetutia aibu katika mechi hii.
Wakati nikitaja mema hayo yaliyokuwapo Tanzania, nilialikwa hapa Nairobi, Kenya nikiwa Rais wa Wahariri Afrika Mashariki (EAES) kushuhudia Uchaguzi wa Jukwaa la Wahariri la Kenya (KEG). Jumamosi ya Aprili 12, 2025 tuliingia ukumbini na uchaguzi wa viongozi hawa haukufanyika. Haukufanyika kutokana na idadi ya wanachama waliohudhuria kutotimiza akidi. Sisi hapo kwetu Tanzania mahudhurio Songea yalikuwa asilimia 98, wao hapa Nairobi yaliishia kuwa asilimia 29, hivyo hawakufikia asilimia 50 inayotakiwa kikatiba kufanya uchaguzi. Tujipongeze sisi wahariri wa Tanzania kwa kuithamini TEF yetu. Hakika tumeijenga TEF imara inayosifika ndani na nje ya nchi. Tumshukuru Mungu kwa hili.
Sitanii, masikitiko ya pili, nikiwa hapa Nairobi nikaona taarifa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amekamatwa mkoani Ruvuma. Lissu, ambaye ni mmoja wa wanasiasa wakosoaji wakubwa wa Serikali, alikamatwa na Polisi akiwa Ruvuma, ila akafikishwa mahakamani Kisutu – Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka mazito ya uhaini — tuhuma ambazo zimewasha moto katika mjadala wa mustakabali wa siasa za vyama vingi nchini mwetu.
Sijasoma jalada juu ya mashitaka aliyofunguliwa Lissu, ila kupitia mitandao na magazeti naona amefunguliwa mashitaka ya uhaini kwa madai ya kutoa matamshi yanayodaiwa kuhatarisha usalama wa taifa na kuchochea uvunjifu wa amani. Maneno hayo yanadaiwa kutolewa kwa nyakati mbalimbali na Lissu, inadaiwa kuwa kauli zake zimetafsiriwa kama kuchochea wananchi kupinga mamlaka halali ya dola. Wafuasi wa Lissu wanapinga vikali tuhuma hizi, wakidai kuwa ni mwendelezo wa mkakati wa kuwanyamazisha wapinzani na kudhoofisha uhuru wa maoni nchini.
Jumapili asubuhi nilipotoka kanisa la Familia Takatifu Basilica Nairobi, nikanunua magazeti matatu; The East African, Sunday Nation na The Sunday Standard. Kichwa cha habari kuu ya Gazeti la The East African kilisomeka: Under siege (Wamezingirwa). Likaweka picha ya kiongozi wa upinzani Uganda, Dk. Kizza Besgye, Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania, Tundu Lissu na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Dk. Riek Machar. Likasema wote hawa wamefunguliwa kesi za uhaini katika nchi zao, ilihali Dk. Machar akiwa katika amri ya kutotoka ndani.

Sitanii, nimesema sijasoma jalada la kesi dhidi ya Lissu. Naona sasa atakula pasaka akiwa rumande, kwani Mahakama ya Kisuti imeahirisha kesi hiyo hadi Aprili 24, 2025. Najua wapo wanaosema acha ashike adabu kidogo. Niseme mapema kuwa hata siku nilipofanya mahojiano na Lissu pale ofisi za CHADEMA Dar es Salaam, nilimpa tahadhari juu ya “kamdomo”. Hakunisikiliza akaishia kutukana, ila nikambana akaomba radhi. Sikubaliani na siasa za matusi, fujo, kutoheshimu sheria na matumizi ya wananchi kama ngao.
Ninachosema matumizi ya wananchi kama ngao, kwa tafsiri ndefu anacholenga Lissu anaposema “No reform, no election,” analenga kuhamasisha watoto wa watu kuingia barabarani. Hajali iwapo wataumizwa au kupoteza maisha kutoka kwa vyombo vitakavyokuwa vinalinda amani na usalama wa wananchi. Nawataka washiriki wa mchezo wa siasa washiriki kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo. Mwaka 2015 Edward Ngoyai Lowassa alipata karibu asilimia 40 ya kura bila kutumia mabavu.
Sitanii, siasa za Tanzania ni za nguvu ya hoja na si za hoja ya nguvu. Kwa majirani zetu hapa nilipo Kenya, kwao matumizi ya nguvu kwenye siasa haikuanza leo. Mwaka 1982 baadhi ya watu walifanya jaribio la mapinduzi, sawa na ilivyotokea kwetu mwaka 1963 au akina Uncle Thom miaka ya 1980 pia kilichotokea sote tunajua. Kenya wanafunzi walimwagika barabarani, polisi waliokuwa wanalinda amani wakawamiminia risasi. Sisi Tanzania walitafutwa viongozi wa uasi, na hakuna Mtanzania aliyeuawa. Kenya wamezoea kuanzia enzi za MAUMAU. Sisi tumedai uhuru kwa amani. Kufikiri Gen-Z itahamia Tanzania na kufanya kazi, ni kujitekenya ukacheka.
Hata hiyo, wakati nikieleza ninachokiwaza kwa uwazi, mwandishi wa Vitabu Mnigeria, Chinua Achebe ametufundisha kupitia fasihi, kwamba sisi wanadamu tunalo jukumu la “kumfukuza mbwamwitu kwanza, kisha tumuonye mwanambuzi asichezee vichakani.” Nafahamu kuna ambao wameifurahia makala hii kabla ya kuanza kusoma aya hii, na kuna ambao wanatamani kunichana kabla ya kusoma aya hii na kuendelea.
Kwa jina la kulinda demokrasi katika nchi yetu, naamini si sahihi mtu yeyote ambaye hajala njama za wazi za kufanya mapinduzi ya serikali kufunguliwa kesi ya uhaini. Narudia, sijasoma jadala kujua Lissu alifanya njama zipi, ila nimeshitushwa na Lissu kufunguliwa kesi nzito ya aina hii. Kila nikisoma makosa aliyotuhumiwa nayo yanaangukia kwenye uchochezi, ila kumpa uhaini? Wahusika wamekwenda mbali mno.
Sitanii, tayari tumeanza kula matunda ya kufungua kesi ya uahini kwa wanasiasa. Tanzania kwa ustaarabu wa Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, si ya kuingizwa katika ligi moja na Uganda au Sudani Kusini katika kuminya demokrasia. Tuliamini enzi za Awamu ya Tano zimekwisha, kumbe bado watesi wapo. Vyombo vya habari vya kimataifa vinavyotuandika juu ya kesi hii tunaweza kuvichukulia kwa wepesi ila mambo kama hayo ndiyo yamefukuza wawekezaji hapa Kenya, wakakimbilia Tanzania kwa wingi.
Nakubaliana na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kwamba CHADEMA kama wameamua kugomea uchaguzi ni haki yao kugoma. Aliliweka vizuri mno hili tukiwa pale Songea kuwa kama hawataki kushiriki uchaguzi wa mwaka huu, waachwe watashiriki 2030, 2040 au 2050 wakati watakapowiwa. Kumfungulia kesi ya uhaini Lissu ni kuipaka matope sura ya Tanzania kuwa hakuna uhuru wa kutoa mawazo au kufanya siasa.

Kukamatwa kwa Lissu kumeibua maswali mazito juu ya mwelekeo wa siasa za Tanzania. Siasa hizi za kupelekana mahakamani kwa tuhuma nzito kama uhaini si tu zinadidimiza uhuru wa kisiasa, bali pia zinatishia mshikamano wa kitaifa. Katika nchi yoyote inayojitahidi kujenga demokrasia imara, matumizi ya sheria kali kama uhaini kwa wanasiasa wa upinzani yanapaswa kuwa ya mwisho kabisa na kwa ushahidi wenye uthibitisho wa hali ya juu. Vinginevyo, hali kama hii inaibua hisia kuwa sheria inageuzwa silaha ya kisiasa, badala ya kuwa chombo cha haki.
Siasa za Tanzania sasa zinaanza kufanana na mashindano ya kumwaga petroli kwenye moto unaowaka. Vyama vya siasa, badala ya kushindana kwa hoja, vinaingia katika mtego wa kutumia nguvu au sheria kali dhidi ya wapinzani wao. Hali hii haina mshindi — kwa sababu kadri hali inavyozidi kuwa tete, ndivyo taifa linavyozidi kusogea katika hatari ya migawanyiko isiyofaa na kutikisika kwa amani ya nchi yetu.
Sitanii, siasa si uadui, bali ni ushindani wa mawazo na sera. Kukamatwa kwa Lissu kwa tuhuma za uhaini kunapaswa kuwa kengele ya tahadhari kwa wanasiasa wote — wa chama tawala na wa upinzani. Taifa linahitaji siasa za uvumilivu, majadiliano, na kuheshimu tofauti za mawazo badala ya siasa za chuki na hofu.
Kwa hakika, iwapo vyama vya siasa vitaendelea kushitakiana kwa tuhuma nzito kama hizi, Tanzania inaweza kujikuta kwenye mtego wa kisiasa ambao utakuwa vigumu kujinasua. Ni wakati wa viongozi wa kisiasa, watunga sera, vyombo vya dola na wananchi kwa ujumla kufikiria kwa kina athari za siasa hizi za kulipizana visasi kwa mustakabali wa taifa letu. Hapa ndipo nawaza kuwa wakati wa kuingia mwafaka kwa wanasiasa wetu umefika. Tusichochee kuni, tuzime moto. Chadema nanyi msimamo wenu wa kukataa mazungumzo mjue hauna hata chembe ya afya. Tusisubiri kupatanishwa, bali tupatane wenyewe. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827