Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limechangia huduma tiba na afya kwenye hospitali ya Jiji la Berberati iliyoko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati tarehe 14 Aprili mwaka 2025.
Akizungumza mara baada ya uchangiaji wa huduma hizo kwa niaba ya Kamanda Kikosi cha Nane cha Ulinzi wa Amani nchini humo Luteni Kanali Theophil Nguruwe, Mkuu wa Operesheni na Utendaji Kivita wa Kikosi hicho Maj Mkangara Mzuma amesema kuwa JWTZ limefanya hivyo ikiwa ni moja ya kuimarisha amani nchini humo.

” Siku zote JWTZ linathamini maisha ya watu na linawajibika na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu”alisema Maj Mzuma.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daktari Sanzema Komoto amelishukuru JWTZ na uongozi wa Kikosi Cha Nane Cha Ulinzi wa Amani nchini humo kwa moyo wao wa kujitolea ili kurudisha amani kwa wananchi wake.
“Tangu JWTZ lianze ulinzi wa amani nchini kwetu, limekuwa msaada mkubwa kwenye kusaidia huduma za afya na wananchi wetu wamefaidika sana” alisema Daktari Komoto.
Huduma tiba na afya zilizotolewa ni uchangiaji wa damu salama, vyandarua, vyakula, sabuni, maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira ya hospitali hiyo.

