Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Wananchi wa vijiji vya Mkenda Nakawale Halmashauri ya Songea vijijini pamoja na wananachi wa kijiji cha Mitomoni Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) Ruvuma kwa kuona umuhimu wa kuwaletea mradi mkubwa wa ujenzi wa daraja la mto Ruvuma uliopo Mitomoni lenye urefu wa mita 45 na barabara zake zenye urefu wa kilomita 8.8.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari waliotembelea kwenye vijiji hivyo walisema kuwa ujenzi wadaraja hilo tayari umeshaanza ambao unaleta faraja kwa wananchi kwani muda mrefu walikuwa na changamoto hiyo ya kushindwa kuvuka kwenye mto mkubwa mto Ruvuma.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Salehe Juma aliyesimama katikati akikaguwa miundombinu ya Barabara ya Mkenda Nakawale kuelekea Mitomoni wilayani Nyasa.

Yasin Idd mkazi wa Mitomoni wilayani Nyasa alisema kuwa jambo ambalo Serikali imelifanya la kujenga daraja hilo la mto Ruvuma litawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa kijiji cha Mitomoni ambao tangu uhuru upatikane kwenye nchi hii walikuwa wakisafiri kwa shida wakati wanapotaka kwenda kupata mahitaji songea mjini ambako ni makao makuu ya mkoa kwani wakati mwingine wamekuwa wakisafiri kwa kutumia mtumbwi jambo ambalo ni hatari hasa ikizingatiwa kuwa mto Ruvuma una mamba wengi.

Yazidu Mohamedi mkazi wa kitongoji cha Mkakawa kata ya Mitomoni akiazungumza na waandishi wa habari kijijini hapo alisema kuwa mradi mkubwa huo wa ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara zake zenye urefu wa kilomita 8.8 unaleta imani kubwa kwa Serikali ambayo imefikia kuwakumbuka wananchi wa vijiji vilivyopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

“Shukrani zetu kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na wabunge wa majimbo mawili haya ya Peramiho wilayani Songea na Nyasa kwani wameleta ukombozi mkubwa sana hasa kwa sisi wananchi ambao tulikuwa tunapata shida kubwa kwenda Songea kutafuta mahitaji au kwenda hospitali kubwa ya Peramiho na Hospitali ya Mkoa Songea .”alisema Mohamed.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma mhandisi Salehe Juma akiwa na msimamizi wa mradi toka TANROADS Mhandisi Fednand Mdoe wakikagua ujenzi wa Blbarabara kwa kiwango cha changarawe.

Rukia Seif mkazi wa kijiji cha Mkenda Nakawale wilayani Songea alisema kuwa watu wengi wekiwemo wanawake wajawazito wamekuwa wakipoteza maisha kwa kuzama kwenye maji baada ya mitumbwi waliyokuwa wamepanda kupinduka hasa kipindi cha masika ambapo mto huo hujaa maji hivyo ameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja hilo ambalo likikamilika litaweza kuwainua kiuchumi wanapotoka vijijini kwenda kuuza mazoa yao kwenye soko la kimataifa lililopo kijiji cha Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambalo watu toka nchi jirani wanaenda kupata mahitaji yao.

Kwa upande wake msimamizi mkuu wa mradi huo toka TANROADS Mhandisi Fedinandi Mdoe alisema kuwa ujenzi wa daraja hilo tayari ushaanza na unatarajiwa kukamilika Septemba 3 mwaka huu na kwamba gharama za mradi ni bilioni 9.293 na mradi huo ulianza Novemba 7 mwaka jana.

Naye Mhandisi Blanka Mkundelinda ambaye ni mkaguzi wa Matirio kwenye mradi huo alisema kuwa vifaa vya ujenzi vipo tayari na baadhi vimeshapelekwa kwenye maabara ya Songea na Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo na vingine tayari vimeshakwenda kwenye eneo la daraja lilioanza kujengwa.

Hata hivyo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Salehe Juma alisema kuwa daraja hilo linajengwa na mkandarasi mzawa kutoka Mkoa wa Ruvuma Wilayani Mbinga Kampuni ya ukandarasi ya Ovans na ujenzi unaenda vizuri kama alivyosema mkandarasi wa kampuni hiyo ambapo aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kuona umuhimu wa kuwa walinzi wazuri kwa kulinda miundombinu ya daraja hilo litakapokamilika pasiwe na watu wachache kujitokeza kuhiujumu miundomingi hiyo kwani inajengwa kwa gharama kubwa .

Alisema mradi huo umefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mfuko dharula na kwamba wafadhili hao wanataka mradi huo ukamilike kwa wakati uliopangwa na hakutakuwa na dirisha la kuongeza muda kwa kuwa fedha zote zimeshapatikana.