Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WMJJWW), Riziki Pembe Juma amesema Wizara hiyo inaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuona upelelezi wa kesi ya Mtuhumiwa Ramadhani Hamza Hussein (28) Mkaazi wa Tomomdo, Unguja anayetuhumiwa kwa kosa la kumdhalilisha mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 inafikishwa Mahakamani ili haki itendeke.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati akimkagua mtoto huyo aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa, Lumumba Zanzibar, baada ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji huko Jang’ombe Mjini Unguja na Mtuhuhumiwa Ramadhani Hamza Hussein.

Waziri Riziki alisema tukio hilo limetokea tarehe mosi, Machi, mwaka huu, na kuripotiwa tarehe 31/03/2025 katika kituo cha Mkono kwa Mkono pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na hatimae kupewa PF3.
Alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano wa kutosha katika kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwani hatua hiyo itasaidia kupunguza vitendo hivyo katika jamii kwani vinaathiri kimwili na kisaikolojia.
Riziki alisema endapo mtu ataona kuwepo kwa viashiria vya aina yoyote ambavyo vitasababisha kutokea vitendo hivyo, ni vyema kuripoti sehemu husika ikiwemo kwa sheha wa shehia husika au kituo cha Polisi kilichopo karibu naye ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa haraka.

“Ukweli suala la udhalilishaji linatuumiza sana wazazi, maana hata mshtakiwa afungwe miaka 100 au kifungo cha maisha, lakini hakiwezi kurudisha thamani na utu wa mtoto wetu, nawaomba wanaume jamani tafuteni watu wazima wenzenu na tuachieni watoto wetu” amesisitiza Waziri huyo.
Mwisho alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwalinda na kuwajali watoto wao, pamoja na kuwafuatilia miendendo yao ili kuwakinga na vitendo vya udhalilishaji kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Kwa upande wa Daktari aliepewa dhamana ya kumshughulikia mtoto huyo Dk. Hasnat Mbarouk Salum alisema mpaka sasa hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri ambapo ametoa wito kwa jamii kuacha vitendo hivyo na kusaidia watoto kukua katika mikono salama ya wazazi na walezi pia.

