Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KAMISHNA Jenerali wa Uhamiaji Dk Anna Makakala, kuna umuhimu wa kuchukua hatua za dhati na za kimkakati ili kuhakikisha kuwa usawa wa kijinsia unakuwa sehemu ya maisha ya kila siku na kuhamasisha wanawake kujitokeza kushiriki katika nafasi za uongozi.

Amesema kuna umuhimu wa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu haki za kijinsia na umuhimu wa fursa sawa kwa wote ili kufikia usawa wa 50 kwa 50 kwa urahisi.

Dk Makakala aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye siku ya jinsia ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), iliyofanyika jana chuoni hapo.

 Dk Makakala alisema kuna umuhimu wa kuhakikisha jamii inaondoa aina zote za ubaguzi wa kijinsia katika elimu, ajira, na uongozi na kuimarisha mifumo ya kisheria na kijamii ya kuzuia unyanyasaji wa kijinsia.

Alisema kuna umuhimu wa kuhimiza wanaume kuwa sehemu ya suluhisho, kwa kushiriki katika mijadala na sera zinazohusu usawa wa kijinsia  na kuwezesha wanawake kiuchumi, kuboresha upatikanaji wa fursa za rasilimali na kuimarisha tafiti na takwimu za kijinsia kwa ajili ya maamuzi sahihi.

“Hatua hizi zinatekelezeka ikiwa sote tutashiriki kwa pamoja katika kuhakikisha kuwa usawa wa kijinsia hauwi tu nadharia, bali unatekelezwa kwa vitendo na napenda kusisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni msingi wa maendeleo endelevu,” alisema.

Alisema kuna umuhimu wa kushirikiana kwa dhati na Serikali katika kuhakikisha jinsia zote zinapata haki sawa na fursa sawa za kushiriki katika maendeleo ya kijamii na kitaaluma.

“Nawaasa mjiamini bila kujali jinsia ili kuzifikia fursa za kiuchumi na kijamii na leo ni siku ya kutafakari tulipotoka, tulipo, na tunapokwenda kwani tunahitaji mshikamano wa kweli, kwa sababu mabadiliko hayaletwi na juhudi za mtu mmoja bali za jamii nzima,” alisema.

Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga alisema CBE imekuwa ikiadhimisha siku ya jinsia kila mwaka ili kuendelea kuhamasisha jamii ya chuo hicho kuzingatia usawa wa kinsia kwenye ngazi za maamuzi.

Profesa Lwoga alisema CBE imejitahidi kwa kiwango kikubwa kuzingatia usawa wa jinsia kwenye uongozi wa chuo hicho na kwamba kimekuwa kikichukua hatua kali kwa watu ambao hawazingatii usawa wa jinsia.

“Kwenye uongozi kuanzia wakuu wa idara kila zinapotokea nafasi na jinsia zote kuwa na sifa zinazojitosheleza tumekuwa tukijitahidi kuweka usawa wa jinsia na hiyo imetufanya tuwe na idadi kubwa ya wanawake kwenye nafasi za uongozi hatujafanikiwa 50/50 lakini tunatakamani kufika huko,” alisema.

Alisema chuo hicho chenye kampasi nne za Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam kwenye udahili wa mwaka huu wamedahili wanafunzi zaidi ya 22,000 na kati ya hao wanawake waliodahiliwa ni 10,000 ambayo ni sawa na asilimia 46.1 ya wanafunzi wote.

“Idadi ya wanaume ni asilimia 53 kwa hiyo chuo kimekuwa kikijitahidi kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapata elimu ya juu kuanzia ngazi ya chuo, shahada, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu na mwaka huu tukipata ithibati tutaanza kutoa shahada ya uzamivu ya infomatiki,” alisema Profesa Lwoga.

Alisema ili kuhakikisha kunakuwa na usawa wa jinsia na kuepusha masuala ya unyanyasaji chuo kimeanzisha dawati la jinsia la wanafunzi na la watumishi wa chuo hicho na madawati hayo yamesaidia kutoa elimu kwa makundi yote.