Ndege za kijeshi za Israeli zimeshambulia jengo la makaazi ya watu katika eneo la kaskazini mwa Gaza lililoharibiwa kwa vita na kusababisha vifo vya takriban watu 23.

Vifo hivyo vimeripotiwa wakati mapigano yaliyoanza upya hivi karibuni katika ukanda huo yakionyesha dalili ya kutopungua.

Hospitali ya Al-Ahly imeeleza kuwa takriban watu 23 wameuawa katika shambulio hilo, wakiwemo wanawake wanane na watoto wanane. Wizara ya afya inayosimamiwa na kundi la Hamas imethibitisha vifo hivyo.

Kwa mujibu wa huduma ya dharura ya wizara hiyo ya afya, shambulio la Israel limelenga jengo la ghorofa nne katika eneo la Shijaiyah, mjini Gaza huku vikosi vya uokoaji vikiripotiwa kuendelea kutafuta manusura chini ya kifusi.

Shirika la ulinzi wa raia, linalofanya kazi chini ya usimamizi wa Hamas, limesema majengo mengine jirani pia yameharibiwa kufuatia shambulio hilo la anga.

Jeshi la Israeli IDF limeeleza kuwa lilimlenga mwanachama mwandamizi wa kundi la Hamas ambaye anasemekena kupanga mashambulizi kutoka Shijaiyah, lakini halikumtaja jina wala kutoa maelezo zaidi kuhusu mwanachama huyo wa Hamas.

Israel inalilaumu kundi la Hamas kwa vifo vya raia wa Palestina kwa sababu wapiganaji wake wanajificha katika maeneo yenye watu wengi.