Timu ya wapatanishi wa Ukraine itasafiri kwenda Marekani wiki hii, wakitarajia kusaini mkataba wa madini ambao umekwama kwa wiki kadhaa.

Washington pia inataka haki za kuchimba madini nchini Ukraine kwa kubadilishana na misaada inayoipa nchi hiyo. Mkataba huo ulitarajiwa kutiwa saini mwezi Februari, lakini Rais Zelenskyy akatoka kwenye ya mkutano wa Ikulu ya White House bila kukubaliana na mpango huo. Hiyo ilitokana na majibizano makali mbele ya kamera za waandishi habari kati yake na Trump na Makamu wa Rais JD Vance.

Ujumbe wa Ukraine mjini Washington utajumuisha wawakilishi wa wizara za uchumi, mambo ya nje, haki na fedha. Jambo moja la kuzingatia katika mpango huo ni msaada unaotolewa kwa Ukraine na Marekani chini ya Rais wa zamani Joe Biden. Zelenskyy anasema hatakubali msaada huo kuchukuliwa kama mikopo ambayo lazima ilipwe. Maelezo kamili ya rasimu ya sasa ya mkataba huo hayajawekwa wazi.