Rais Donald Trump amesema Marekani itaanzisha mazungumzo, ya ngazi ya juu na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia siku ya Jumamosi. Alitoa tangazo hilo la kushangaza alipokutana na Netanyahu katika Ikulu ya White House.
Rais huyo wa Marekani alisema ana matumaini ya kufikia makubaliano na Tehran, lakini akaonya kuwa jamhuri hiyo ya Kiislamu itakuwa katika “hatari kubwa” kama mazungumzo hayo yatashindwa.
Saa chache baadae, Tehran ilithibitisha kuwa mazungumzo yanatarajiwa Jumamosi mjini Oman, lakini ikasisitiza kuwa “hayatakuwa ya moja kwa moja”. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameandika kwenye mtandao wa X kuwa mpira sasa uko upande wa Marekani.
Trump hakusema ni wapi mazungumzo hayo yatafanyika, lakini alisisitiza kuwa hayatahusisha watu wengine na yatakuwa ya “ngazi ya juu zaidi.”
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa katika Ikulu ya White House na Rais Donald Trump, Makamu wa Rais JD Vance na Mshauri wa Usalama wa Taifa Michael Waltz.Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa katika Ikulu ya White House na Rais Donald Trump, Makamu wa Rais JD Vance na Mshauri wa Usalama wa Taifa Michael Waltz.
Tangazo la Trump limejiri siku moja baada ya Iran kutupilia mbali mazungumzo ya moja kwa moja juu ya mkataba mpya wa kuudhibiti mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, ikilitaja wazo hilo kuwa lisilo na maana.
Rais huyo wa Marekani alijiondoa katika mkataba wa mwisho mwaka 2018, wakati wa urais wake wa kwanza. Wakati huo huo, maafisa wamesema kuwa Urusi, China na Iran zinatarajiwa kufanya mashauriano kuhusu suala la nyuklia la Iran hii leo Jumanne mjini Moscow.
Kauli za Trump zimejiri wakati Netanyahu akiwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kusihi kibinafsi kuondolewa kwa ushuru wa Marekani ambao umeutikisa ulimwengu.
Waziri Mkuu huyo wa Israeli aliahidi kuondoa “vikwazo vya kibiashara” kati ya nchi hizo mbili. Kabla ya mkutano huo, nchi yake ilichukua hatua ya kuondoa ushuru wake wa mwisho uliosalia kwa bidhaa za Marekani.
