MVUA kubwa iliyonyesha kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa imewauwa karibu watu 30 na kusababisha kuharibu mkubwa katika mji huo mkubwa. Watu wengine wamejeruhiwa vibaya na kuhamishiwa kwingine.

Waziri wa Afya ya umma wa moa wa Kinshasa Patricien Gongo Abakazi amesema kuna watu wengi waliojeruhiwa ambao wamehamishiwa sehemu nyingine.

Waliokufa walizama majini au kuangukiwa na kuta za nyumba zao zilizoporomoka. Baada ya mvua kubwa kunyesha Ijumaa usiku kuamkia Jumamosi, mafuriko yaliharibu vitongoji vya mji huo wenye wakaazi milioni 17.

Baadhi ya wakazi walilazimika kusafiri mjini humo kwa kutumia mitumbwi. Mafuriko aghalabu husababisha hasara kubwa mjini Kinshasa, mji ulioko kwenye kingo za Mto Kongo, ambao ndio wa pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Mto Nile. Gavana wa Kinshasa Daniel Bumba Lubaki amesema miundo mbinu ya maji imeathirika lakini huduma zitarejeshwa ndani ya siku mbili au tatu.

Mto Ndjili, ambao unapita katika sehemu ya mji huo, ulifurika na kuvunja kingo zake Ijumaa usiku na kuiziba barabara kuu ya kitaifa. Mtaalamu wa masuala ya maji Dk. Raphael Tshimanga Muamba alisema mto huo umeathiriwa na shughuli za binadamu kwa muda.

Katika wilaya ya mashariki ya Debonhomme, maji yaliyasoma magari, na kuwalazimu wakaazi kuogelea au kutumia mitumbwi. Baadhi ya waathiriwa walinasa kwenye sehemu za juu za nyumba zao baada ya maji kujaa kwenye ghorofa za chini.

“Maji yamefikia urefu wa mita moja na nusu. Tumefanikiwa kujiokoa, wengine wamekwama majumbani mwetu,” alisema Christophe Bola, mkazi wa mtaa wa Ndanu katika wilaya ya Limete.

Mafuriko hayo yalisababisha msongamano mkubwa wa magari katika mji ambao foleni ni hali ya kawaida. Katika mwaka wa 2022, kiasi ya watu 120 walipatikana wamekufawakati wa mafuriko kama hayo mjini Kinshasa.

Afrika ya Kati imekuwa ikikumbwa na mvua kubwa ikiandamana na radi tangu Alhamisi wiki iliyopita, na hasa nchini Guinea ya Ikweta na Gabon.