Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejizatiti kukabiliana na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa ili kulinda uhai wa wananchi na mali zao.

Haya yalisemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akikagua uzio wa umeme wenye urefu wa kilomita zipatazo 33 unaotumika kutatua changamoto ya wanyama wakali na waharibifu kwa kutenganisha Pori la Akiba Ikorongo na vijiji vipatavyo 06 katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Kitandula alifanya ziara hiyo kwa lengo la kukagua ufanisi wa uzio huo na kujionea manufaa yanayopatikana kwa wananchi wa vijijini vinavyopakana na uzio huo.

Katika ziara hiyo Kitandula hakusita kuwataka wahifadhi kuendelea kubuni njia nyingine zenye tija za kutatua changamoto ya wanyama wakali na waharibufu kwa kuwa serikali ina wajibu mkubwa wa kulinda uhai wa wananchi na mali zao, sambamba na kuendeleza Uhifadhi wa Maliasili hizi tulizopewa na Mwenyezi Mungu kama zawadi.

“ Taifa limetukabidhi Wizara ya Maliasili na Utalii jukumu kubwa na zito la kulinda maliasili zinazohusisha wanyama, malikale na misitu kwaniaba ya Watanzania. Sambamba na jukumu hilo tunao wajibu vilevile kwaniaba ya serikali kuhakikisha uhai na mali za wananchi wanaozunguka maeneo ya Hifadhi vinalindwa. Hivyo lazima tutumie maarifa kupata majawabu ya changamoto inayolisumbua Taifa kwasasa ya wanyama wakali na waharibifu na wakati huo huo maliasili nazo zilindwe ili ziendelee kuchangia katika uchumi wa nchi yetu” alisema Kitandula.

Kitandula aliongeza kuwa Serikali ipo tayari kuingiza maeneo mengine nchini yenye changamoto ya wanyama wakali na waharibifu kwenye matumizi ya teknolojia ya uzio wa umeme, hatahivyo alisema matumizi hayo lazima yaongozwe na ushauri wa kisayansi, hivyo amewataka wahifadhi wafanye tafiti na kuja na ushauri wa kisayansi utakaowezesha kuanzishwa matumizi ya ya uzio wa umeme katika maeneo mengine nchini.

Aidha, alihimiza wahifadhi kuendeleza matumizi mchanganyiko ya mbinu mbalimbali za kisasa katika kusaidia kulinda maliasili za wanyamapori na kuondoa changamoto ya migongano ya wanyama wakali na waharibifu. Alihimiza kuongezeka kwa matumizi ya ndege nyuki, mabomu baridi, uvishaji wa mikanda ya mawasiliano, uvunaji wa wanyama wakorofi, na matumizi ya kamera kwenye uzio wa umeme ili kuuongezea ufanisi.

Uzio wa umeme katika Pori la Akiba Ikorongo ulijengwa mwaka 2019 na Kampuni ya Grumeti Reserves (T) Ltd kwa idhini ya Wizara ya Maliasi na Utalii. Uzio huo wenye urefu wa Kilometa 33 umejengwa ndani ya mpaka wa Pori la Akiba Ikorongo bila kugusa maeneo ya vijiji. Mpaka huo unapita katika vijiji sita (06) vinavyopakana na pori hilo ambavyo ni Mbilikili, Bonchugu, Rwamchanga, Kazi, Miseke na Park Nyigoti katika Wilaya ya Serengeti.