Na Magrethy Katengu,JamhuriMedia
Dar es Salaam
Katika jitihada za kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi Serikali imezindua mfumo wa kidigitali unaowezesha kutambua maeneo yenye samaki na kutoa taarifa za masoko.
Mfumo huo ujulikanao kama ‘Potential Fishing Zone’ (PFZ) umebuniwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI).
Akizungumza Aprili 3,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mfumo huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Edwin Mhede, amesema mfumo huo ni muhimu kwa kuwa utaokoa muda na rasilimali zingine zinazotumika katika shughuli za uvuvi.
“Baada ya majaribio ilionyesha wazi asilimia 75 ya waliotumia programu hii hawakufanya uvuvi haramu, mfumo uliwaonesha waende wapi wakavue, kwahiyo ni muhimu sana kwa sababu utaokoa muda, utaokoa rasilimali zingine zinazotumika kuendesha boti kama mafuta, utahakikishia mtu anavua samaki ambao wanahitajika sokoni,” amesema Dk. Mhede.

Aidha amesema watu wanaporasimishwa kupitia mfumo huo inakuwa rahisi kuwatambulisha kwenye taasisi nyingine zinazotoa huduma kusaidia maendeleo ya sekta ya uvuvi zikiwemo taasisi za fedha.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dk. Ismael Kimirei, amesema mfumo huo umetengenezwa kuiwezesha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukusanya taarifa na kuwawezesha wavuvi kufikia maeneo mazuri yenye samaki na kuuza kwa bei ya ushindani.
“Tunaahidi kuendelea kuboresha mifumo hii ili iweze kuchukua mazao zaidi na kuiwezesha sekta ya uvuvi kukua kwa kasi na kuchangia katika uchumi wa nchi,” amesema Dk. Kimirei.
Baadhi ya wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Soko la Kimataifa la Samaki Ferry wamesema mfumo huo utawezesha kupanua wigo wa biashara zao.
“Tumeufurahia sana kwa sababu ni mfumo wa kisasa ambao utawafikia watu wengi mikoani hadi nje ya nchi,” amesema Omary Regan.
Mvuvi mwingine Shabani Ramadhani amesema mfumo huo utaongeza upatikanaji wa samaki tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wakivua kwa kubahatisha.
“Tulikuwa tunaenda baharini kwa kuomba Mungu tu, hujui samaki yuko wapi lakini sasa hivi hatutabahatisha tena kwa sababu mfumo unakuonyesha samaki walipo,” amesema Ramadhani.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mfumo huo pia utarahisha utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa kuwa taarifa zote za wavuvi zitapatikana kidigitali.
Aidha amesema wataendelea kuboresha Soko la Kimataifa la Samaki Ferry ili lizidi kuwa la kisasa na kwamba wametenga zaidi ya Sh milioni 300 ili kuboresha miundombinu mbalimbali sokoni hapo.
Mpaka sasa wavuvi na wauzaji 915 wamejisajili katika mfumo huo na miamala 9,000 ya zaidi ya Sh milioni 100 imefanyika.