Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea

KATIBU Mkuu na Mgombea Mwenza Mteule wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amesema kitendo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutaka kususia uchaguzi mkuu ni haki yao kisheria.

Hayo ameyasemwa leo Aprili 4, 2025 wilayani Songea mkoani Ruvuma wakati wa uzinduzi wa Mkutano Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), DK Nchimbi alisema Tanzania imekuwa na utaratibu wa kufanya uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano na imekuwa ikifanya hivyo tangu mwaka 1960.

“Tangu mwaka 1960 Tanzania imekuwa ikifanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano na ifikapo wakati wa uchaguzi hakuna raia yeyote anayeweza kusema uchaguzi usifanyike,.

“Hata Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu, hawezi kulitamkia taifa kuwa uchaguzi hautafanyika kwa sababu hili ni takwa la kikatiba.” amesema Nchimbi.

Dk Nchimbi aliwahakikishia wahariri na Watanzania wote kuwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025 utafanyika.

“Lakini pia nitumie nafasi hii kusisitiza kwamba pamoja na haki ya raia kugombea na kuchaguliwa ni kosa kubwa kukilazimisha chama chochote cha siasa kuingia kwenye uchaguzi.”

“Zimeanza kusikika taarifa mbalimbali za baadhi ya wananchi na wanaCCM wakishinikiza CHADEMA iingie kwenye uchaguzi, ni haki yao kususia, na uchaguzi huu sio wa mwisho.

“Kwa hiyo niwape salamu ndugu zangu wa CHADEMA rafiki yangu Tundu Lissu na wenzake nawapa salamu na watu wasiwaonee bure, uchaguzi huu sio wa mwisho kuna mwingine 2030, kuna mwingine 2035, kuna mwingine 2040 wakiukosa huu wataupata ule mwingine.”

“Mtu yeyote asiwalazimishe CHADEMA kuingia kwenye uchaguzi ni haki yao kutoshiriki uchaguzi na kwa mujibu wa Katiba yetu chama hata kikiwa kimoja kikijitokeza wananchi watapiga kura ya ndio au hapana kwa hiyo kukaa kuwasemasema CHADEMA kila siku si sawa ni kinyume cha katiba na kinyume cha sheria.

“Kwa hiyo namuambia rafiki yangu huko aliko Tundu Lissu ana haki kabisa na chama chake kutokugombea na tutawaunga mkono chochote watakachoamua, kugombea na kutogombea ni haki yao na ikitokea hawatagombea basi watukumbuke kwa kura.” amesema.

Aidha, Dk Nchimbi alipogeza Jukwaa la Wahariri kufauata katiba yake kwa kufanya uchaguzi na kusisitiza kuwa hatua hiyo inawafanya kuwa mfano wa kuigwa kwa taasisi ambazo hazina utaratibu wa kufanya changuzi kulingana na katiba zao.

“Mnatukumbusha sisi wote wajibu wa pekee tulionao wa kuhakikisha tunafuata katiba na taratibu zetu, uchaguzi unachangia kuleta mabadiliko katika taasisi na taasisi zisizofanya uchaguzi zinafubaa, zinachakaa na mwisho zinakufa.”

Alisema zipo taasisi zisizo za kiserikali zaidi ya nusu hazifanyi uchaguzi hatua ambayo inazidumaza na kushindwa kusonga mbele.

Dk Nchimbi alisema pia TEF imekuwa mstari wa mbele kuboresha mahusiano ya kijamii na kuzisemea 4R za Rais Samia Suluhu Hassan na kuifanya jamii kukubaliana na kuwa na vyombo vya habari huru.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Songea Mjini, Dk Damas Ndumbaro aliwahakikishia wanachama wa Jukwaa la Wahariri kuwa Serikali ya Rais Samia itashikamana na kushirikiana na waandishi wa habari ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo.

“Jukwaa la wahariri na waandishi wa habari ni kundi muhimu sana, hivyo niwaombe ushirikiano wa kuwajulisha watanzania mambo ya kweli na sahihi ambayo Serikali imeyafanya katika kuchochea nchi iweze kusonga mbele maendeleo na kimataifa.”

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanal Ahamed Abbas alisema Mkoa huo ni moja ya mikoa minne inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini na unachangia pato la taifa kwa asilimia 3.8.