Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umesema kuwa Matumizi ya teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwaajili
ya ujenzi wa barabara na madaraja imeweza kupunguza gharama zaidi ya 50.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga wakati akifungua semina ya Waandishi wa habari kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TARURA.

Amesema WAKALA huo umeweka kipaumbele cha kutumia malighafi zinazopatikana maeneo
ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi.
“Katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala tunaendelea kufanya majaribio kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madaraja ya mawe ‘stone arch
bridges’ pamoja na teknolojia nyingine katika kuboresha barabara tunazozisimamia.
“Matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya madaraja, huongeza ufanisi, huokoa muda,
hutunza mazingira kwa gharama nafuu,” amesema.
Mhandisi Mkinga amefafanua kuwa, Wakala unaendelea na matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana maeneo ya kazi na utafiti wa teknolojia mbadala za ECOROADS, Ecozyme na GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira.

Aidha Mhandisi Mkinga amesema Wakala umeimarisha upitikaji wa miundombinu ya barabara za wilaya zenye urefu wa kilometa 5,057.765 kwa asilimia 55 kitaifa na asilimia 52 Kimkoa huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 60 ifikapo Juni, mwaka huu.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ongezeko kubwa la bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 25.431 hadi shilingi bilioni 52.334 sawa na ongezeko la asilimia 205.79 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/25.
“Mtandao wa barabara za lami katika kipindi hichi umeongezeka kutoka Kilometa 469.47 hadi Kilometa 636.519, na changarawe kutoka Kilometa 1,327.55 hadi Kilometa 1,686.706 huku
barabara za udongo zimepungua kutoka Kilometa 3,260.75 hadi Kilometa 2,731.54 kwa mapato ya ndani,” amesema Mhandisi Mkinga.









