Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani
SERIKALI imetoa maagizo matano kwa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache, ikiwa ni sehemu ya jitihada ya kuboresha ufanisi wa taasisi wanazoziongoza.
Maagizo hayo yaliyotolewa wilayani Kibaha, mkoani Pwani katika mkutano wa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache ni pamoja na kuangalia namna ya kukumbatia mageuzi ya kidijitali, pamoja na utawala bora utakaopelelekea uwajibikaji, uwazi na uongozi unaozingatia maadili.

Pia katika orodha ya maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ni kuja na mikakati ya kuongeza faida, kuongeza ushirikiano na sekta binafsi, pamoja na kuoanisha mikakati yao ya kibiashara na vipaumbele vya kiuchumi vya Taifa.
“Ninatoa changamoto kwenu kutimiza majukumu yenu kama wakurugenzi wa kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache,” amesema Prof Mkumbo wakati wa mkutano wa siku tatu ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuwaleta pamoja washiriki wapatao 150.
“Tunapaswa kuja na mikakati thabiti ambayo itaboresha utendaji wa kampuni ambazo ziko chini ya uangalizi wetu,” amesema Prof Mkumbo.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni zile ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
Jumla ya uwekezaji wa Sh86.3 trilioni umefanywa katika taasisi hizo, huku kati ya kiasi hicho Sh2.9 trilioni zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache na Sh83.4 trilioni kikienda kwa taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100.
“Tunataka tuone matunda ya uwekezaji huu na ndio maana nawataka mfanye kila liwezekanalo kuongeza ufanisi wa taasisi zenu,” amesema Prof Mkumbo, huku akizishukuru taasisi ambazo tayari zinachangia vizuri katika Mfuko Mkuu wa serikali.
Amesesma mchango wa kampuni hizo linapokuja suala la gawio umekuwa ukikuwa kwa kasi nzuri.
Prof Mkumbo amesema gawio ambao serikali inapata kutoka kwa kampuni hizo umeongeza kwa asilimia 236 mwaka wa fedha 2023/24 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Amesema gawio liliongezeka kutoka Sh58 bilioni mwaka 2019/20 hadi kufikia Sh195 bilioni mwaka 2023/24.
“Hii ni ishara ya uthibitisho wa nia ya dhati ya kampuni hizo kuunga mkono jitihada za serikali chini ya uongozi thabiti wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akifanya kazi usiku na mchana kutengeneza mazingira rafiki ya biashara,” amesema Prof. Mkumbo.
Amezitaka kampuni hizo kuendelea kuchangia zaidi ili kutimiza lengo la serikali la kuongeza mapato yasiyo ya kikodi kutoka kwa taasisi inazomiliki kwa asilimia 100 na zile inazomiliki kwa hisa chache.
Serikali imejidhatiti kuongeza mapato hayo kutoka asilimia tatu za sasa hadi kufikia asilimia 10 ndani ya kipindi cha miaka mitano.Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida, alieleza dhamira ya serikali ya kuendelea kutengeneza mazingira rafiki ya biashara ili kuongeza mchango wa taasisi zake na zile ambazo ina umiliki wa hisa chache.

“Tunatarajia kuzindua mpango wa pili wa maboresha ya mazingira ya biashara ‘blueprint’ wiki ijayo ikiwa ni ishara ya dhamira ya serikali ya kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini” alisema Dk Kida.
Ameongeza: “Tunataka kuainisha changamoto za wakati huu na kuzitatua ili kuchochea uwekezaji nchini,” amesema.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema mkutano huu unalenga kutoa nafasi ya majadiliano kuhusu mchango wa teknolojia linapokuja suala la maamuzi yatokanayo na data (“data-driven decision making”) na ufanisi wa taasisi.
“Ni katika muktadha huo, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaona haja ya wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali ina hisa chache kukumbatia mageuzi ya teknolojia.
“Tanzania sio kisiwa, hivyo, wakurugenzi wetu wanapaswa kujiandaa kuongoza taasisi zao kwa kutumia maono yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia ulimwenguni,’ amesema Mchechu.
Mkutano wa mwaka huu na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache unakuja katika wakati ambapo teknolojia ina jukumu muhimu katika kuimarisha uchumi wa taifa.

Mchechu amesema matarajio yake ni kwamba kupitia majadiliano, watatengeneza mazingira bora kwa maafisa watendaji wakuu na wakurugenzi ili waweze kutumia teknolojia kwa ufanisi na hivyo kuongeza tija ya taasisi wanazoziongoza.
Naye Lightness Mauki, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina anayesimamia Utendaji, Ufuatiliaji na Tathimini-Mashirika ya Kibiashara, alisema kwamba kwa kipindi cha miaka minne iliyopita gawio kutoka kwa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache limekuwa likikuwa kwa wastani wa asilimia 50 kila mwaka.
“Naamini mchango wa kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache unaweza kuongezeka mara dufu kwa mwaka huu wa fedha kwani takwimu za hivi karibuni zimekuwa zakuridhisha.

“Tunachukua jitihada mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa muongozo wa bodi za wakurugenzi za kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, tukio lililofanyika leo,” amesema.
Ameongeza kuwa, muongozo huo umeeleza wazi namna wakurugenzi wa bodi wanapaswa kutimiza majukumu, huku matarajio ya serikali yakiwa ni kuona ufanisi wa kampuni hizo na mchango kwa serikali unaongezeka.




