Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita
Mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Kakoyoyo iliyopo wilayani Bukombe Mkoa wa Geita, Ibrahim Masumbuko (9) amefariki dunia baada ya kupigwa na radi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adamu Maro, amethibitisha taarifa hiyo kwa waandishi wa habari akieleza kuwa tukio limetokea Machi 23, 2025 katika kijiji cha Kakoyoyo mkoani humo.
Amesema siku ya tukio, ilinyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na radi na kuwajeruhi watoto wengine wawili wa familia moja ambao ni Kulwa Masumbuko (11) mwanafunzi wa darasa la tatu na Isaka Masumbuko (03).
Maro amesema wakati wa tukio watoto hao walikuwa kwenye mashamba ya mpunga wakiwinda ndege, na baada ya kuona mvua kubwa walianza kukimbia kurudi nyumbani wakiwa njiani ndipo walipigwa na radi.
“Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi, huku waliojeruhiwa wamepatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Bulega na kuruhusiwa na hali zao zinaendelea vizuri.
“Jeshi la Polisi linawaasa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi cha mvua ili kujiepusha na kujikinga na madhara au athari zinazoweza kujitokeza,” amesema Kaimu Kamanda Maro.
Kaimu Kamanda Maro amesema elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi wote kuhakikisha wanachukua tahadhari ya kujikinga na matukio ya radi ikiwemo kuepuka kukaa maeneo yenye miti mingi nyakati za mvua.
