Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

WAFANYABIASHARA wilayani Songea mkoani Ruvuma wameiomba Benki ya CRDB kutoa elimu zaidi kuhusu mkopo wa kilimo ili waweze kufaidika na huduma hiyo kwa ufanisi zaidi na kuongeza uzalishaji wenye tija na si vinginevyo. 

Ombi hili linakuja kutokana na changamoto zinazowakumba wakulima na wafanyabiashara wa kilimo katika kupata taarifa za kutosha kuhusu masharti ya mikopo, vigezo vya kupata mikopo, na faida zinazoweza kupatikana. 

Wafanyabiashara hao wametoa ombi hilo jana kwenye Semina ya siku moja iliyowezeshwa na Benki ya CRDB  kwa wafanyabiashara na wajasiliamali 300 wa Mkoa wa Ruvuma yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Anglikana manispaa ya Songea.

Meneja wa benki ya CRDB Tawi la Songea Ruwaich Minja akizungumza kwenye semina ya wafanyabiashara mjini Songea

 Jastin Nguruwe mkazi wa Mjimwema manispaa ya Songea alisema kuwa yeye kama Mkulima ,anawashauri benki  ya CRDB kutoa elimu ya mkopo kwa wakulima ambayo itawasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo na kuongeza uzalishaji, huku wakitafuta njia za kufanikisha maendeleo ya sekta hiyo.

“Niwaombe watu wa benki ya CRDB elimu hii ya mkopo wa kilimo waitoe kwanza kwa wakulima kwani wakulima walio wengi wanakuwa na haraka ya kukopa inapofika wakati wa marejesho inakuwa ngumu kwa kuwa ile pesa wamefanyia matumizi mengine kama kujengea nyumba ” alisema.

Costantine Kessy mkulima na mfanyabiashara alisema kuwa kwenye mafunzo hayo amefurahishwa na jambo moja ambalo linamlinda mfanyabiashara pale anapoweza kukopa na baadae akapata changamoto ya kiafya au biashara ukitoa taarifa mapema wanaweza kukufutia mkopo wako.

“Vilevile mkopo wa kilimo unamwezeshwa mkulima kumiliki maghala au kuwa na usafiri ambao unaweza kupeleka mazao yake sokoni kwa wakati kwa hiyo CRDB wamesema wanauwezo na wanatoa ushirikiano tena kwa asilimia 120 ya mlengwa na asilimia 80 CRDB wenyewe wanajazia ili mteja aweze kufanikisha malengo yake kwa wakati.” Alisema.

Baadhi ya wafanyabiashara wakishiriki semina iliyotolewa na Benki ya CRDB juu ya fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa na benki hiyo.

Fina Fuko mkulima kutoka Wilaya ya Namtumbo amesema kuwa mafunzo hayo yatamsaidia zaidi kwenye kilimo chake cha matunda na ili aweze kulima kwa viwango vikubwa na kukidhi mahitaji ya wateja katika soko anahitaji kupata mtaji mkubwa na anatamini apate mtaji wa vifaa hasa vifaa vya umwagiliaji ili aweze kulima matunda yake kwa mwaka mzima.

 ” Mafunzo haya na maelezo ambayo nimeyapata naona kwamba ndogo yangu ya kuwa mkulima mkubwa wa matunda inaenda  kufanikiwa kwa hiyo nna wahimiza watu wote ambao wanawaza kwamba kilimo au biashara gani hawezi kupata mkopo au mtaji basi wafike CRDB waweze kupata mikopo na hivyo kutimiza ndoto zao.” Alisema 

Naye Emmanuel Biganio meneja Biashara kanda ya kusini wa benki ya CRDB alisema kuwa kanda yao wanahudumia mikoa mitatu Lindi,Mtwara na Ruvuma ,kwa Mkoa wa Ruvuma wameweza kutoa Mafunzo hayo kwa wajasiliamali na wafanyabiashara ili kuweza kufahamishana fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki hiyo.

Alisema kuwa lengo ni  namna wanavyoweza wakabadilisha Biashara zao kutoka hali iliyopo sasa na kwenda hali ambayo ni ya juu zaidi na bila mtu kufahamu fursa au kupata taarifa za nini ambacho kinapatikana ndani ya CRDB anaweza akashindwa kupiga hatua kwa haraka.

“Mathalani Benki ya CRDB ni Benki pekee ambayo imepewa idhini na Global finance fund ya kuwekeza kwenye miradi ya kijani na kwa Africa ni Benki tatu na Tanzania ni Benki ya CRDB tu,sasa taarifa hizi kama tusipoeleza vizuri wajasiliamali ambao wanajihusisha na shughuli ambazo zinatunza mazingira itakuwa sio rahisi wao kutumia fursa hii ambapo inamitaji ya kutosha lakini pia inatoa tekinolojia za kutosha ambazo zitahararakisha biashara zao.”alisema  Biganio.

Emmanuel Biganio Meneja Biashara Kanda ya Kusini akitoa mada kuhusiana na mkopo wa kilimo kwa wadau na wafanyabiashara wa Wilaya ya Songea.

Peter Christopher Meneja wa mradi wa program za kilimo endelevu kutoka CRDB makao makuu alisema kuwa wameanzisha mradi wa TACATDP ambao unalenga kusaidia wakulima wenye changamoto za athari ya mabadiliko ya tabia nchi na itasaidia wakulima wengi kupata mikopo ya riba nafuu ambayo itawasaidia kutumia mbinu au zana za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Kwa upande wake Ruwaich Minja meneja wa Tawi la CRDB Songea alisema kuwa wamepata fursa ya kutoa mafunzo kwa wadau wao mbalimbali, wateja wao katika Mkoa wa Ruvuma ni mafunzo ambayo wao kama benki wameona ni fursa waende kwa wananchi ili wazungumze nao na kuwaonesha fursa ambazo CRDB wanazitoa  kwenye maeneo mbalimbali lakini katika Wilaya ya Songea ambayo ipo kimkakati katika kujihusisha na kilimo.

“Tumeona tuweke semina ambayo itawakusanya wafanyabiashara wakubwa na wadogo, lakini pia tutawapata wakulima na wadau mbalimbali ambao wanakuwepo katika mnyororo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo letu hili la Songea.” Alisema Minja.