Urusi na Ukraine zimekubaliana kusitisha mapigano katika Bahari Nyeusi katika mikataba tofauti na Marekani, baada ya siku tatu za mazungumzo ya amani nchini Saudi Arabia.

Serikali ya Washington ilisema pande zote zitaendelea kufanya kazi kuelekea “amani ya kudumu ” katika taarifa zinazotangaza makubaliano hayo, ambayo yatafungua tena njia muhimu ya biashara.

Pia wamejitolea “kubuni hatua” za kutekeleza marufuku iliyokubaliwa hapo awali ya kushambulia miundombinu ya nishati ya kila upande, Ikulu ya White ilisema.

Lakini Urusi ilisema usitishaji vita wa majini utaanza kutekelezwa tu baada ya vikwazo kadhaa dhidi ya biashara yake ya chakula na mbolea kuondolewa.

Maafisa wa Marekani wamekuwa wakikutana kando na wapatanishi kutoka Moscow na Kyiv mjini Riyadh kwa lengo la kusuluhisha mapatano kati ya pande hizo mbili. Wajumbe wa Urusi na Ukraine hawajakutana moja kwa moja.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema makubaliano ya kusitisha mapigano katika Bahari Nyeusi ni hatua katika mwelekeo sahihi.

“Ni mapema mno kusema kwamba yatakuwa ya ufanisi, lakini hii ilikuwa mikutano sahihi, maamuzi sahihi, hatua sahihi,” aliuambia mkutano wa waandishi wa habari huko Kyiv.