Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu. Wiki iliyopita nimezungumzia suala la ukomo wa wabunge wa viti maalum na nikaisihi serikali iangalie uwezekano wa kutanua wigo ukomo uende na kwenye viti vya majimbo. Kwa sasa wabunge wa viti maalum ndiyo watakaokuwa na ukomo wa vipindi viwili; yaani miaka 10. Nimependekeza hata wabunge wa majibo uwekwe ukomo wa miaka 15. Nimepata mrejesho mkubwa.

Sitanii, naomba niwe mkweli kwa nafsi yangu. Wapo wabunge ambao ubunge wao hauna ungamano na wananchi, bali wamegandishwa kwa gundi ya uji. Sina uhakika kama sitawataja mwanzo hadi mwisho wa makala hii, kwani wengi nao wanajifahamu. Kura za maoni walipata namba za viatu, na bahati mbaya hata majimboni kwao hawajafanya kitu.

Mbunge mmoja tu, ambaye pamoja na kupata namba ya viatu katika kura za maoni, angalau amepunguza kero moja. Mbunge huyu nilipata kumshauri asigombee tena. Nilieleza sababu zitakazomwangusha. Lakini angalau kama nilivyosema, baada ya hapo kero moja ameelekea kuitatua; Barabara ya Nyangoye, Bukoba. Mnyonge mnyongeni, ila haki yake mpeni.

Huyu ni Stephen Byabato, Mbunge wa Bukoba Mjini, ambaye angalau amewezesha mlima wa Nyangoye ambao umekuwa chimbuko la ajali kwa miaka mingi, amewezesha umekatwa. Lipo la Stendi, ambalo bado yeye anasema itajengwa huko Nyanga, ila washindani wake wanasema huo ni mfupa mgumu kwake. Lipo la uhusiano wake na viongozi wenzake, hilo namwachia apambane nalo mwenywe.

Mkoani Shinyanga, Mbeya, Kilimanjaro, Kigoma, Arusha na Dar es Salaam, yapo majimbo ambayo tayari yamewekwa rehani. Kwa leo siyataji kwa ujumla wake, ila msomaji ukihesabu vidole unayafahamu moja baada ya jingine. Sisi wapigakura, nia yetu si kuona mtu anashindwa, maana hatufaidiki lolote kwa mbunge kushindwa, ila akichagua mwenywe kushindwa sisi ni akina nani hadi tumzuie?

Sitanii, niruhusuni nimguse mmoja angalau wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaha. Akiwa Waziri wa Ardhi, alitwambia hana shida ndogo ndogo, angalau sasa anatumia chenji aliyoiacha babu yake. Kwa kweli kwa unyenyekevu mkubwa sisi wakazi wa Kata ya Kitunda, Ilala, Dar es Salaam, hakika tumemkinai mbunge wetu. Barabara ya Kitunda – Banana, kila mwaka anatupiga ‘sound’.

Imefika wakati sisi wakazi wa Kitunda tumemkumbuka Dk. Makongoro Mahanga. Mungu amlaze mahala pema peponi. Akiwa mbunge wa Ukonga, Dk. Mahanga na Meya Abuu Jumaa, walianzisha ujenzi wa Barabara ya Banana – Kitunda. Barabara hii yenye urefu wa kilomita 4, kilimota ya kwanza ilijengwa vizuri sana. Bahati mbaya nasikia wakubwa walimnyima kandarasi ya pili mjenzi huyu kumalizia kilomita 3 za lami kipande Hali ya Hewa (Viwanja vya Ndege) – Kitunda.

Mkandarasi aliyepewa kilomita tatu za kona ya Hali ya Hewa hadi Kitunda, kipande chote cha kilomita tatu alichojenga mwaka 2015, lami iliishaisha na bila aibu, Halmashauri ya Jiji walileta greda wakakwangua lami na kuweka kifusi. Kifusi kilichowekwa kwa miaka minne sasa kimechimbika mashimo hadi abiria kwenye bajati mvua ikinyesha maji yanaingia ndani na kuvuka kima cha kiti walichokali; wanaloana makario!

Sitanii, inawezekana Silaa amewatende mema kata nyingine za Ukonga, ila kwetu Kitunda atavuna alichopanda. Tunavisikia vijimaneno vyake, eti kila anayemsema anatangaza alimwomba vijisenti akamnyima. Sisi wengine tunamshukuru Mungu, kwani hatujawahi kumwomba atoe japo sadaka, achilia mbali mchango wa harusi. Ni kwa mantiki hiyo napata ujasiri wa kumweleza Silaa kuwa sisi hatumdai pesa, tunataka barabara. Hapa Ukonga – Kitunda, tunasema No Road, No Silaa.

Tumezichoka ahadi hewa. Tunalipa kodi. Rais Samia Suluhu Hassan amejenga barabara za vijijini, lakini kwa udhaifu wa mbunge wetu, sisi tuko katika Jiji la Dar es Salaam, ila tunaishi kama ndege mkiwa juu ya mti. Katika hili tunasema hapana. Uchaguzi wa mwaka huu uwe wa ajenda. Tunahitaji mgombea katika Jimbo la Ukonga au majimbo yote nchini, ajipime na aahidi atatutendea nini. Hatutaki ahadi hewa.

Sitanii, nilidhamiria kutotaja majina, ila sisi tuliozaliwa enzi za TANU tunayo ahadi namba 8 ya mwana – TANU inayosema: “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.” Mdogo wangu huyu ninayemzidi zaidi ya muongo mmoja, nimeambiwa haambiliki. Najua inawezekana sikio la kufa halisikii dawa, ila hapa kwetu Kitunda tumelishana yamini. Tusitafutane ubaya, heri mimi nimesema. Kitunda tunasema No Road, No Silaha. Urafiki wetu ni wa maendeleo si wa kukogana. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827