📌 Unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa hadi Sumbawanga
📌 Kapinga asema Mkoa wa Rukwa kuunganishwa na gridi ya Taifa kupitia mradi wa TAZA
📌 Serikali yatoa Bilioni 21.4 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi
📌 Wananchi Wilaya ya Mufindi kunufaika na mitungi ya Ruzuku
Serikali imesema kuwa, itaukamilisha kwa wakatil mradi wa kuziunganisha na gridi ya Taifa mchi za Tanzania na Zambia (TAZA) unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kutokana na umuhimu wa mradi huo wa kuunganisha Mkoa wa Rukwa na gridi ya Taifa ambao hivi sasa unatumia umeme wa mafuta ya diseli.
Hayo yameelezwa leo machi 19, 2025 na Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kukagua utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Kisada Iringa ambacho ni sehemu ya mradi huo.

“Miradi ambayo inafanyika na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kweli ni miradi ya kimkakati, Mheshimiwa Rais aliahidi mkoa wa Rukwa nao kuingia kwenye gridi ya Taifa kupitia mradi huu”. Amesema Mhe. Kapinga
Ameongeza kuwa, mradi wa TAZA ni muhimu katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme ndani ya Nchi huku akitolea mfano Mkoa wa Songwe ambao baadhi ya maeneo yyanapata umeme mkoa wa Mbeya na laini kuwa imetembea umbali mrefu hivyo kusababisha changamoto za upatikanaji wa umeme.
Serikali imetoa takribani Shilingi Bilioni 21.4 kwa ajili ya malipo kwa
wananchi 6,279 ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi.
Aidha, wananchi 5,929 sawa na asilimia 94.43 wamelipwa na Serikali inaendelea na malipo kwa wananchi waliobaki.

Kuhusu nishati safi ya kupikia Mhe. Kapinga amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Mufindi kunufaika na mradi wa mitungi ya Ruzuku ambayo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaitoa kwenye kila Wilaya nchini.
Amesema kwa kila Wilaya kunamitungi takribani 3,255 ambayo itapatikana kwa bei ya ruzuku ya nusu bei ya shilingi 20,825 kutoka shilingi 45,000 kwa mtungi mmoja.
Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha umeme wa uhakika na unaotabirika unawafikia wananchi wote ili waweze kunufaika kwa shughuli za kiuchumi.






