Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imefurahishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ambao umechochea uboreshaji wa huduma katika bandari mbalimbali hapa nchini uliotokana na maboresho ya uwekezaji.
Akizungumza mara baada kufanya ziara ya kujionea utendaji kazi katika maeneo mbalimbali ya bandari ya Dar es Salaam , Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Seleman Kakoso (Mb) alisema kuwa wameshuhudia maboresho makubwa ya utendaji kazi katika bandari mbalimbali ikiwemo ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga na ujenzi wa bandari kavu katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam.

“Tunaipongeza TPA kwa usimamizi na uboreshaji mzuri wa bandari baada ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuvutia uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali ya bandari na kutoa pesa nyingi kwa ajili ya ujenzi wa bandari nyingine ikiwemo ya Mbamba Bay katika ukanda wa Ziwa Nyasa unaogharimu mabilioni ya shilingi za Kitanzania,” amesema Bw. Kakoso.
“Maboresho haya ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu kwa sababu bandari ni lango kuu la uchumi wa nchi na inaiwezesha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kupata kodi ya kutosha kwa ajili ya mipango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Bw.Kakoso.
Akizungumzia maboresho yaliyofanyika katika bandari ya Dar es Salaam wakati wa majumuisho ya ziara ya Kamati hiyo, mheshimiwa Kakoso amesema wamejionea maboresho makubwa ikiwemo idaidi ya meli kuongezeka baada ya muda wa meli kushusha mizigo kupungua tofauti na ilivyokuwa zamani kabla ya uwekezaji mkubwa kufanyika.
“ Tumefurahishwa sana na maboresho makubwa katika bandari ya Dar es Salaam ikiwemo mipango ya maboresho ya miundombinu kama vile uboreshaji wa mfumo wa umeme, upanuzi wa kina na upana wa lango la meli kupitia mpango mkubwa wa maboresho ya miundombinu ( Dar es Salaam Maritime Gateway Project-DMGP).”
“Maboresho haya ambayo yanafanywa na wawekezaji ikiwemo DP World yanawapa nafasi TPA ya kuweka nguvu zaidi katika maboresho ya bandari nyingine kama vile Mtwara, Tanga zikiwemo na bandari kavu kama vile Kwala (Pwani) na Uhumwa (Dodoma) ili kuipunguzia mzigo bandari ya Dar es Salaam isielemewe,” amesema Bw Kakoso.

Bw.Kakoso amesema ujenzi wa bandari kavu utasaidia kulinda miundombinu ya barabara na kupunguza foleni kwa sababu malori yanayopelekea mizigo bandari ya Dar es Salaam hayatalazimika tena kuingia katika jiji hilo.
Kupitia mpango wa DMGP, Bw.Kakoso pia ameitaka TPA kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi kuharakisha mpango wa ujenzi wa reli inayoingia katika bandari hiyo ili kubeba mizigo na kupeleka katika bandari kavu .
Kamati hiyo ya Bunge pia imeishauri TPA kununua maeneo ya kutosha ya hifadhi ya mamlaka hiyo kwa ajili ya upanuzi zaidi wa bandari katika miaka ijayo.

“Bandari zote kubwa duniani zinakuwa na hifadhi kubwa ya ardhi kwa ajili ya upanuzi wa katika miaka ijayo,”
“Hivyo, kamati inaishauri TPA itenge fedha za kuwalipa wananchi fidia ili kununua maeneo yaliyo karibu na bandari kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za bandari;” amesema.
Akiongea katika ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Daktari Bw.Baraka Mdima amesema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi, wawekezaji na wadau wengine katika uboreshaji wa huduma katika bandari mbalimbali ikiwemo ya Dar es Salaam ambayo inahudumia nchi mbalimbali za jirani ikiwemo Rwanda, Burundi, DR Congo, Zambia, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa wizara hiyo Bw David Kihenzile amempongeza Rais Samia kwa kuruhusu uwekezaji mkubwa katika bandari ya Dar es Salaam uliopelekea maeneo mbalimbali ya uboreshaji huduma ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kisasa.
“Matokeo haya tunayoyaona yanatokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuweka mazingiza bora ya kuvutia wawekezaji na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na uboreshaji wa bandari mbalimbali hapa nchini” alisema Bw Kihenzile.
Naye Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam Bw Gallus Abed alisema uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam umeleta mabadiliko makubwa katika ufanyaji kazi wa bandari hiyo ambapo hivi sasa muda wa meli kushusha mizigo umepungua kutoka wastani wa siku 7-10 hapo awali mpaka siku tatu za hivi sasa.
