Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Kupitia mfumo wake wa ruzuku ya mbolea,imesaidia ongezeko la matumizi ya mbolea kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024.
Ongezeko hilo limewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 za virutubisho kwa hekta mwaka 2020/2021 hadi kilo 24 za virutubisho kwa hekta mwaka 2024/2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo (TFRA), Joel Laurent ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 19, 2025, katika Ofisi za jijini Dodoma.

Amesema lengo ni kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2033 kwa kuzingatia makubaliano ya Wakuu wa Nchi za Afrika yaliyofanyika Nairobi 2024.
Amesema kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini kumechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 19,980,718 mwaka 2020/2021 hadi tani 22,803,316 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 14 na kufanya utoshelevu wa chakula nchini kufikia asilimia 128.
“Katika miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya mbolea nchini imepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwa na mafanikio makubwa ambayo yamechangia kuimarika kwa kilimo, biashara ya mbolea, na uwekezaji katika viwanda vya mbolea, ” ameeleza.
Amefafanua kuwa Mpango huo maalumu wa ruzuku ya mbolea umewezesha kupunguza gharama ya mbolea na kufanya wakulima kununua mbolea kwa bei ya shilingi 40,000/= hadi 80,000/= kwa kutegemea aina ya mbolea na umbali sawa na punguzo la takribani asilimia 50 ya bei.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne,biashara ya mbolea nchini imekua kwa kiasi kikubwa ambapo wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 hadi 7,302 Februari, 2025.
Aidha upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/2021 hadi tani 1,213,729 mwaka 2023/2024, uingizaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/2021 hadi tani 728,758 mwaka 2023/2024 na uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 mwaka 2020/2021 hadi tani 158,628 mwaka 2023/2024.
“Ili kusogeza huduma kwa wakulima, Mamlaka imeanzisha Maabara ya kisasa ya mbolea ambapo Tanzania inakuwa Nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Maabara mahususi ya mbolea yenye uwezo wa kupima sampuli za mbolea, udongo na tishu za mimea,
Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha udhibiti wa ubora wa mbolea nchini.
Aidha, maabara hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania, kama vile Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, na Rwanda, “amefafanua
Katika kusogeza huduma kwa jamii, Mkurugenzi huyo amesema Mamlaka imeongeza Ofisi za Kanda kutoka kanda tatu (3) 2020/2021 ambazo ni Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini hadi kufikia Kanda tano (5) mwaka 2023/24 ambapo Kanda ya Kati na Kanda ya Mashariki zimeongezeka.
Aidha amesema , Mamlaka imeajiri Wawakilishi katika Mikoa yote 26 ili kusogeza huduma katika ngazi ya Mkoa.