Urusi na Ukraine zimeanzisha mashambulizi ya anga ambayo yaliharibu miundombinu ya kila mmoja wao, saa chache baada ya Rais Vladimir Putin kusema Urusi itaacha kuyalenga maeneo ya nishati ya Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema malengo ya Urusi ni pamoja na hospitali na vifaa vya umeme. Alisema kiongozi huyo wa Urusi amekataa usitishaji vita kamili katika mazungumzo yake ya Jumanne na Rais wa Marekani Donald Trump.
Putin alimwambia Trump usitishaji kamili wa mapigano utafanya kazi tu ikiwa washirika wa Ukraine wataacha kutoa msaada wa kijeshi – hali ambayo washirika wa Ukraine wa Ulaya wamekataa hapo awali.
Maafisa katika eneo la kusini mwa Urusi la Krasnodar walisema kuwa shambulio la ndege isiyo na rubani ya Ukraine ilisababisha moto mdogo kwenye ghala la mafuta.
Akizungumzia mazungumzo ya simu ya Trump-Putin, Zelensky ameema: “Leo, Putin kimsingi alikataa pendekezo la kusitisha mapigano kamili, Itakuwa sawa kwa ulimwengu kukataa majaribio yoyote ya Putin kuibua vita.”
Ametoa wito kwa washirika wa Ukraine kuendelea kutoa msaada, na pia kuiwekea vikwazo Urusi.
