Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Machi 11, 2025 Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa taarifa ya mabadiliko yaliyofanywa na Halmashauri Kuu ya CCM Machi 10, 2025. Mabadiliko yaliyotangazwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wapiga kura za wagombea katika nafasi ya udiwani, ubunge na ubunge wa viti maalum. Kwa kweli idadi ya wapiga kura za maoni imeongezwa kwa kiwango ambacho wahongaji sasa matumbo yako moto.

Sitanii, kuna majimbo ambayo idadi ya wajumbe wa kura za maoni inakwenda kuwa wajumbe 8,000. Nafahamu baadhi ya wagombea walikuwa wanahonga kati ya Sh 20,000 hadi 500,000 kutokana na uzito wa mjumbe. Ila idadi ya wajumbe maeneo mengi ilikuwa haizidi 400. Leo Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan hapana shaka rushwa katika kura za maoni inamkera na ndiyo maana ameamua kuongeza idadi ya wapigakura za maoni.

Kwa wagombea wa viti maalum pia kwa vijana, nako CCM imechomoa betri. Wapigakura wanaume wamepogeza sifa za kupigia kura wagombea wanawake kwenye kundi hilo. Tuhuma za rushwa ya ngono zilikuwa nyingi katika kundi hili, hivyo nako sasa dawa imepatikana. Watachaguana kina dada wenyewe, hivyo yale makundi ya “mbwa mwitu” hayana lake tena. Napongeza mabadiliko haya kwa dhati.

Mabadiliko makubwa yaliyonigusa ni ukomo wa wabunge wa viti maalum. Kwamba sasa akiishaingia bungeni kupitia dirisha hili, atakuwa na nafasi ya vipindi viwili tu, na baada ya hapo hatakuwa na sifa za kugombea tena ubunge kupitia dirisha hilo. Nawapongeza CCM kwa kuliona hilo ndani ya chama. Kuna wabunge wamekuwa viti maalum miaka 30 sasa. Niombe pia mabadiliko haya yaende kwenye Katiba ya nchi na sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani itamke hivyo.

Ugonjwa wa Viti Maalum kuwa vya kudumu upo si kwa CCM pekee, bali hata kwenye vyama vya upinzani. Kina mama wanaopata nafasi hizi, hawakubali kutoka bungeni. Naamini sasa uamuzi huu umeleta dawa sahihi itakayotoa mwanya kwa watu wengine kujifunza siasa kupitia viti maalum, viwe na maana kweli badala ya sasa vinapokejeliwa na kuitwa “vitu maalum”. Viti maalum viliwekwa kuwapa uzoefu wanasiasa akina mama kisha baada ya hapo waende majimboni.

Sitanii, safari moja uanzisha nyingine. CCM kama mlivyoliona hili la viti maalum, nashauri hata ubunge wa majimbo uwe na ukomo. Mbunge wa jimbo aruhusiwe kugombea si zaidi ya vipindi vitatu mfululizo. Mimi leo nina umri wa miaka 53, lakini kuna wabunge wako kwenye majimbo nimeanza kuwasikia nikiwa darasa la kwanza miaka 46 iliyopita.

Napita kwenye majimbo yao sioni cha maana walichokifanya. Kuna watoto wanazaliwa wanadhani jina la mbunge fulani ni sawa na dini. Hawajawahi kuona mbunge mwingine. Akijitokeza kijana msomi akalitaka jimbo anapigwa “mziziology” na “mziziology” ukimshindwa, anatengenezewa kesi ya ubakaji au mapenzi kinyume na maumbile. Mwisho ukiuliza binti anayedai kufanyiwa ukatili anasema ilikuwa teksi nyeupe, gari likiletwa kwenye ushahidi linaonekana ni la bluu!

Kwa hakika hakuna watu hatari kama wabunge waliokaa kwenye majimbo zaidi ya miaka 20. Huyu ni vigumu mno kumshinda. Kwanza ana “Kamati ya Ufundi”, lakini pili ana fedha za viinua mgongo vya mabunge manne na uwezekano wa kupata mikopo benki akasambaza rushwa, ni mkubwa. Hata kama hafanyi maendeleo ya aina yoyote kwa wananchi, huyu anao uwezo wa kuhonga hata wajumbe 20,000 akaendelea kushinda. Tuwaangalie sana hawa ni hatari, hasa wasioletea wananchi wao maendeleo.

Sitanii, ya ukomo wa hawa masulutani wa majimbo, najiuliza hawa viti maalum tunaowawekea ukomo wa miaka 10 watakwenda wapi kwani wa majimbo wanasema majimbo yana wenyewe? Tena wengine wanaokuja na fikira mpya wanaitwa “ngedere” na kwamba wanavamia mashamba. Kwa nia ya kufungua mianya, huko nako kwenye majimbo tuweke ukomo wa miaka 15.

Ningependekeza 10, lakini nasema ukomo wa miaka 15 kwa nia ya kuwapa nafasi wabunge waliopo serikali ikimaliza miaka 10, basi serikali inayoingia inufaike na uzoefu wao kwa miaka mitano, baada ya hapo waondoke nao wakaendeshe kilimo kwanza. Ushauri wanaotoa kwa serikali wakiwa mjengoni wakauweke kwenye vitendo wafanye biashara, waendeshe kilimo au wafundishe vyuoni.

Ikiwa mbunge anayeondolewa alikuwa mtumishi mwema, ikiisha miaka mitano aombe tena ubunge wanachi kama wanampenda watamchagua tu. Kwa utaratibu wa sasa hata kama wananchi hawampendi mbunge, ikiwa ana “connection” kumwondoa ni kazi. Nasema hata ubunge wa majimbo mwisho iwe miaka 15 kuanzia sasa, wawapishe wa viti maalum. Naomba kutoa hoja. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827