Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani ameweza kutekekeza miradi yote ya kimkakati iliyoasisiwa na watangulizi wake ikiwemo ya Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametimiza ahadi aliyoitoa kwa Watanzania mara alipoingia madarakani ya kuwa hakuna mradi utakaosimama chini ya uongozi wake na kwamba ataendeleza kila kilichoanzishwa na watangulizi wake.

Amesema hayo leo Jumanne (Machi 18, 2025) alipozungumza katika Kongamano la kumpongeza Mheshimiwa Rais DKt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wake lililoandaliwa na Waandishi wa Habari Mahiri wa Mkoa wa Mwanza kwenye ukumbi wa Tunza jijini Mwanza.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia alipotoa hotuba yake ya kwanza bungeni aliahidi kuwa miradi yote itaendelezwa na mingine mipya itaanzishwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia amefanikiwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na ya huduma za jamii inayowagusa wananchi wote hadi vijijini kwenye sekta za afya, elimu na maji “wote ni mashahidi wa mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa na Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo”

Kuhusu sekta ya maji Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hivi sasa Serikali inatekeleza miradi kwenye maziwa, mito na Mabwawa kwa ajili ya kuwapelekea wananchi wenye uhitaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini.
Aliitaja mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida, Dodoma na Mara kuwa itakayonufaika na miradi wa maji ya Ziwa Victoria Alisema miradi kama hiyo iko pia katika mikoa ya Geita na Kagera.
Kuhusu afya Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imewekeza katika miundombinu ya kutolea huduma za afya, dawa na vifaa tiba kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa, lengo likiwa ni kusaidia kupunguza adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu kupata huduma za afya ikiwemo za kibingwa.
Kuhusu nishati ya umeme amesema wilaya na vijiji vyote vimepatiwa umeme na hivi sasa Serikali inasambaza umeme kwenye vitongoji na visiwa ili kuhakikisha kwamba kila nyumba anamoishi Mtanzania inafikiwa na huduma ya umeme.

Akizungumzia kilimo Mheshimiwa Majaliwa amesema zao la pamba ambalo awali uzalishaji wake ulikuwa umezorota Serikali imeimarisha mifumo ya masoko ya zao hilo kwa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umepandisha bei ya zao kilo.
Amesema hivi sasa zao la hilo limerudi kwenye nafasi yake ya kuwa moja kati ya mazao makuu ya biashara nchini na viwanda vingi vya kuchambua pamba vimejengwa hasa mkoani Simiyu.
Kuhusu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuteuliwa kuwa mgombe wa Urais wa CCM Katie uchaguzi mkuu ujao, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amefurahishwa na kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Michael Lushinge kuwa mkoa huo utaongoza tena kwa kumpiga kura nyingi za ndiyo mgombea Urais wa CCM.
Akitoa mada katika kongamano hilo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kagosa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alianzia Kanda ya Ziwa kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR ya kutoka Mwanza kwenda Isaka lengo likiwa ni kuifanya Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa Ukanda wa Maziwa Makuu.
Naye Mratibu wa kongamano hilo, Aloyce Nyanda amesema kuwa kwa namna yoyote kazi zinazofanywa na Serikali zina manufaa makubwa kwa wananchi ndiyo maana yeye na waandishi wenzake wa habari wameamu kujadili mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia kama kiongozi wa mkuu wa nchi na mtumishi wa watu.


