Serikali imesema itaendelea kumuenzi Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi ametoa ahadi hiyo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Lukuvi alitoa ahadi hiyo Machi 17 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Mzeyi, Mlima wilayani Chato mkoani Geita wakati wa ibada ya Misa Takatifu ya kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha Dk Magufuli.

Dk Magufuli aliaga dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.
Lukuvi alisema serikali inatambua mchango wa Dk Magufuli kwani tangu mwaka 1995 amehudumu kwenye nafasi tofauti ikiwemo ya ubunge, naibu waziri, waziri na rais.
“Dk Magufuli alikuwa mzalendo wa taifa lake, kiongozi aliyejali watu na rasilimali za nchi yake, mcha Mungu,” alisema Lukuvi.
Mtoto wa Rais Magufuli, Jesca Magufuli ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuenzi mema yaliyofanywa na baba yao na kuendelea kuwa karibu na familia.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Nicolous Kasendamila alisema ni muhimu taifa lienzi misingi ya Magufuli kwa kulinda amani na umoja.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella alihimiza wakazi wa Geita na Chato waendelee kuishi misingi ya uchapakazi na kuilinda miradi inayoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi alihimiza watumishi wa taasisi za umma na binafsi wamuenzi kwa vitendo Dk Magufuli kwa kuimarisha uwajibikaji na kuishi kwa hofu ya Mungu.
Askofu Niwemugizi alisema Dk Magufuli aliipenda nchi yake kwa kulinda rasilimali za nchi, alikuwa mzalendo wa kweli na siku zote alisisitiza kuwajali na kuwahudumia Watanzania wanyonge bila ubaguzi.
Alisema kila mtumishi kwa nafasi yake anapaswa kuwajibika, kukataa mambo mabaya, unyanyasaji, uonevu, lakini kutiana moyo, kuwa na huruma na upendo wa dhati kwa watu wengine.

“Magufuli alisema kuna wanyonge, masikini lazima tuwahudumie hawa, ndo hapo alipokuwa anahimiza watumishi wa umma wawajibike kuangalia watu wa hali ya chini,” alisema Askofu Niwemugizi.
Aliongeza: “Basi hii ni sababu kubwa ya kumuombea na kumkumbuka Magufuli, lakini pia sababu nyingine ya kuwaombea na kuwakumbuka marehemu ni imani ya kiroho, tukumbushane kwamba kifo kipo”.
Alisema Magufuli pia alihimiza viongozi wote kujua Mungu yupo na kutambua kifo kipo na hivyo kuongoza kwa kumtanguliza mbele Mwenyezi Mungu ili kuyaishi yaliyo mema daima.
“Tuliona alivyoaga dunia, watu walivyokuwa wanagalagala njiani, wengine wanazimia kwa sababu ya vile walivyomuona alivyowasaidia na alivyowagusa kwa namna mbalimbali. Mimi naendelea kumkumbuka na kumuombea, na kila mwaka nitakuwa hapa, kwa hiyo tuendelee kumuombea, apumzike kwa amani lakini pia familia yake Mungu awaimarishe,” alisema Askofu Niwemugizi.