Mmoja wa wataalamu wakubwa wa afya nchini Tanzania, Profesa Mohamed Janabi, ametangazwa rasmi kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika.

Prof. Janabi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ni miongoni mwa wagombea watano, ambao majina yao yatafanyiwa mchakato wa Uchaguzi Mei 18, mwaka huu.

Prof Janabi ni mgombea pekee kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, huku wagombea wenzake wanne wakitokea nchi za Afrika Magharibi.

Wagombea hao ni Dk. N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast), Dk. Dramé Mohammed Lamine (Guinea); Dk. Boureima Hama Sambo (Niger) na Pr Mijiyawa Moustafa wa Togo.

Prof Janabi na wenzake wanawania kuziba nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mteule wa Kanda hiyo, Dk. Faustine Ndugulile, waziri wa wa zamani wa afya Tanzania, aliyefariki ghafla Novemba 2024.

Mkurugenzi wa Kanda antachaguliwa kwa kura ya siri katika kikao cha ndani cha Kamati ya Kanda ya WHO kwa Afrika, ambayo ilikutana Januari 14, 2025, na kuamua kutumia utaratibu wa haraka, kumpata Mkurugenzi wa Kanda badala ya mchakato wa kawaida ambayo huchukua muda mrefu.