Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa nchi, ofisi ya Waziri Mkuu ,Kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu, Mhe: Ridhiwani Kikwete ameitaka bodi ya wadhamini ya mfuko wa taifa wa uhifadhi jamii nchini NSSF kusimamia mpango mkakati wa mfuko unaozingatia uboreshwaji wa huduma ya wanachama, michango, uwekezaji na kulipa mafao.

Aidha pia Waziri Kikwete ameitaka bodi hiyo kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Sheria, sera na miongozo inayotolewa na serikali.

Akizungumza pia Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba amesema kuwa huo unaendelea kutimiza azma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe: Rais Dkt: Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii na kuwafikia wananchi waliojiajiri waweze kujiunga na kuchangia ili wanufaike na mafao mbalimbali yanayotolewa na mfuko.

Akiongeza mkurugenzi huyo amesema kuwa suala la wananchi kujiunga na kuchangia katika mifuko ya uhifadhi ya jamii ni ajenda ya dunia na ya nchi na kuwa lipo kwenye ilani ya uchaguzi wa chama, ambapo serikali ya awamu ya sita imelipa umuhimu wa kupekee.

“Ninashukuru Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo umelishikia bango jambo hilo, umeshirikiana na sisi tangu tuanze kampeni yetu ya “NSSF staa wa mchezo” kuhakikisha waliojisajili wanakuwa sehemu ya hifadhi ya jamii kama ambavyo nchi zilizoendelea zimewasajili wananchi waliojiajiri.” alisema.

Hayo yamejiri wakati wa uzinduzi wa bodi ya wadhamini ya NSSF hafla iliyofanyika hapo jana, Machi 14, 2025 jijini Dar es Salaam.