Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SERIKALI imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yao, viwanda na wabunifu ili kufanikisha maendeleo katika sekta ya nguo na mavazi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, katika Kongamano la kujadili maendeleo na changamoto zinazoikabili sekta hiyo lililoandaliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kuelekea maadhimisho ya miaka 30.

Amesema asilimia kubwa ya wanaojihusisha katika sekta hiyo hawana kiwango kikubwa cha elimu lakini wanao ujuzi na ubunifu mzuri katika kutengeneza bidhaa zinazovutia.

“Tunawahitaji sana katika kuimarisha ujuzi tunaoutaka, kwani itawasaidia wanafunzi wetu kujifunza kwa vitendo kupitia nyinyi. Naipongeza VETA kwa kuandaa kongamano hili, na endeleeni kujenga mahusiano mazuri na wadau hawa muhimu.

“Ndoto ya serikali na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha tunazalisha bidhaa zenye ubora kwa wingi ili tuuze ndani na nje ya nchi,” amesema Profesa Mkenda.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore amesema lengo la kongamano hilo ni kukutana na kujadili namna VETA inaweza kushirikiana na wadau hao ili kuendeleza sekta hiyo.

“Mada mbalimbali zimewasilishwa katika kongamano hili na katika kujadiliana tumeona wadau ni wengi na soko ni kubwa, hivyo tunatakiwa kulitumia ili kuzalisha bidhaa za kutosha,” amesema.

Mbunifu wa Mavazi, Miriam Ekilwa amesema: “Tunafurahi hatua ya serikali kutambua umuhimu wetu. Ni matarajio yetu ushirikiano huu unafanyika kwa vitendo ili kuikuza sekta hii muhimu,”.