Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema kuwa nchi yake iko tayari kusitisha mapigano na Ukraine, lakini anasisitiza kuwa suluhisho hilo lazima lilete amani ya kudumu na kushughulikia chanzo halisi cha mgogoro huo.

Putin aliyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa na kiongozi wa Belarus, Alexander Lukashenko.

Kremlin, kwa upande wake, imetangaza kuwa iko katika hatua za mwisho za operesheni ya kuiondoa Ukraine kutoka maeneo iliyoyateka huko Kursk.

Wakati huohuo, mjumbe wa Donald Trump, Steve Witkoff, yuko Moscow kwa mazungumzo na Urusi kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano kwa muda wa siku 30.

Putin alihoji ufanisi wa hatua hiyo akisema, “Nani atatoa amri ya kusitisha mapigano, na itakuwa na thamani gani?” Pia aliuliza ni nani atakayeamua wapi “ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unaweza kutokea,” akimaanisha mpaka wa kilomita 2,000 kati ya Urusi na Ukraine.

Alisisitiza kuwa “masuala haya yanahitaji uchambuzi wa kina na mazungumzo ya kina kati ya pande zote mbili.”

Hata hivyo, Putin alisema kuwa “wazo la kusitisha mapigano ni zuri, tunaliunga mkono, lakini kuna mambo kadhaa yanayohitaji kujadiliwa.”

Akaongeza kuwa anaamini majadiliano na Marekani na washirika wake ni muhimu, akisema kuwa “huenda” atafanya mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani, Donald Trump.

“Tunaliunga mkono kabisa wazo la kumaliza mgogoro huu kwa njia za amani,” alihitimisha.