Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze

WAKAZI wa vijiji vya Kitonga, Milo, na Buyuni, kata ya Vigwaza, Jimbo la Chalinze, mkoani Pwani, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ubovu wa barabara, hali inayowapa usumbufu mkubwa.

Aidha, baadhi ya wakulima wameeleza kukerwa na changamoto ya wafugaji kulisha mifugo kwenye maeneo yao, ambapo wanadai kuwa wafugaji wanapewa kipaumbele, jambo linalosababisha wakulima kushindwa kulima kwa hofu ya mazao yao kuharibiwa na mifugo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti ,wakazi wa kijiji cha Milo walisema kuwa ni muda mrefu hawana barabara ya uhakika.

Mzee Rashid Thabit, Masahafu Mgweno, Malki Paulo, Hadija Ally, na Adam Mohammed walieleza , tatizo la barabara linazidi kuwa kubwa na wanaomba Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuisimamia kabla mvua hazijaanza kunyesha.

Kuhusu changamoto ya wakulima na wafugaji, Hadija alifafanua kuwa asilimia 80 ya wakazi wa kijiji cha Milo ni wakulima.

“Tunashindwa kulima, ardhi ipo hatarini, Tumeshafika mara kadhaa kutoa taarifa kwa serikali ya kijiji, lakini hatujaona msaada, Tunaiomba serikali ya wilaya na mkoa kutusaidia.”

Vilevile, alieleza changamoto kubwa ya maji yasiyo salama, akidai maji wanayotumia ni kutoka kwenye mabwawa, ambapo wanachangia pia kunywa na mifugo ya ng’ombe, jambo ambalo silo jema kiafya.

Katika kijiji cha Buyuni, Mtumwa Mhoja, James Mlewa, Abdul Adinan, na Seif Mrisho walisema wanakabiliwa na changamoto za migogoro ya ardhi na eneo la Narco ambapo wamesema wapo kwenye maeneo hayo kwa kipindi kirefu.

Mzee Mtumwa Mhoja alieleza kuwa, tangu mwaka 2007 mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge (MKURABITA) ulitekelezwa kijijini Buyuni, ambapo walikubali kutenga maeneo ya wafugaji.

“Hata hivyo, mpango huu haukukamilika kutokana na kitabu cha sheria ya MKURABITA kutokuwa na saini ya viongozi wanne wanaotakiwa, Hivi sasa tunataka maeneo yetu, maana wafugaji wanaacha mipaka yao na hawaheshimu wakulima,” alisema Mzee Mhoja.

Aliongeza kuwa, kwasasa wananchi wanadai maeneo yao na kufikia 2022 walifika wilayani Bagamoyo, ambapo walielezwa kufuatilia shauri hilo kwa ofisa ardhi wa mkoa, lakini hadi sasa hawajapata majibu yoyote.

Kuhusu changamoto ya barabara ya Vigwaza-Buyuni, Adinan alisema barabara hiyo ina urefu wa km 9,ingawa imechongwa, bado haikidhi, wanaomba iboreshwe.

Akijibu changamoto ya barabara, Meneja wa TARURA wilayani Bagamoyo, Mhandisi Bupe Angetile, alieleza kuwa barabara ya Kitonga-Milo yenye urefu wa km 11 ilitengwa milioni 497 kwa mwaka 2023/2024 na inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.

Bupe alisema mkandarasi anaendelea na kazi ya kufukia makaravati madogo kabla ya kuanza kuchonga barabara.

Kuhusu barabara ya kijiji cha Buyuni, Bupe alifafanua kuwa wananchi walikuwa wameomba barabara ichongwe ili iweze kupitika, na kazi hiyo imekamilika, lakini bado wameomba maombi maalum ya fedha kwa ajili ya kuimarisha barabara hiyo, na mchakato wa maombi unaendelea.

Katika changamoto za migogoro ya ardhi na mipaka ya wakulima na wafugaji, Ofisa Ardhi wa Chalinze, Baltazar Mitti, alieleza kuwa changamoto kuu ni ukosefu wa uelewa wa sheria za ardhi miongoni mwa jamii.

“Nimebeba kero hizi, naahidi kuzifikisha halmashauri na tutakuja kuzungumza na wananchi kuhusu masuala ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji, na jamii kwa ujumla,” alisisitiza Baltazar.

Diwani wa kata ya Vigwaza, Mussa Gama, alieleza kuhusu changamoto za migogoro ya ardhi zinazohusiana na Narco, akisema kuwa eneo lote linamilikiwa na Narco, lakini serikali iliidhinisha eneo la hekari 1,200 kwa ajili ya wananchi.

“Tatizo kubwa ni wananchi kutokuhamia kwenye maeneo waliyopewa na serikali na wengine kuuza maeneo hayo na kutaka kubaki kwenye maeneo ya zamani, jambo linaloharibu utaratibu,” alisema Gama.