Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mkuranga
Baadhi ya vijana walioajiriwa katika viwanda vinavyomilikiwa na raia wa China wilayani Mkuranga, Pwani wameeleza changamoto wanazokutana nazo kazini, ikiwamo ukosefu wa mikataba, vifaa vya kujikinga pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamesema uwapo wa viwanda nchini ni fursa lakini pia ni changamoto kutokana na matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo.
Wamedai changamoto kuu inayowakabili kwa sasa ni ukosefu wa mikataba ya kazi katika baadhi ya viwanda vya kampuni inayoendeshwa na raia wa Kichina, pamoja na ukosefu wa vifaa salama vya kujikinga dhidi ya madhara.
Aidha, wamesema kuna mikataba isiyolingana na hali halisi, matumizi ya nguvu, na kunyimwa uhuru wa kupata chakula wakati na likizo.
JAMHURI imethibitisha kuwapo kwa changamoto hizo zinazowafanya vijana wengi kukumbana na unyanyasaji wa masilahi kutoka kwa wawekezaji.
Aidha, vijana wengi wanaofanya kazi katika viwanda hivyo hawana elimu ya kutosha kuhusu haki zao, hasa wanapokumbana na ubaguzi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Dundani, Issa Uya, amesema vijana wanaofanya kazi katika viwanda vya wawekezaji kutoka China wanakumbana na changamoto mbalimbali za mikataba, vifaa vya kujilinda na unyanyasaji.
Amesema wawekezaji hao wanatoa ushirikiano mdogo, hali inayosababisha vijana wengi kukosa msaada wanapokutana na matatizo katika viwanda hivyo, hasa wakati wanapojaribu kutafuta msaada ofisini kwake.
“Nimekwisha kujaribu kuwafuata wawekezaji hao wamekuwa hawataki kushirikiana, wamekuwa wakijiona wana nguvu zaidi za mamlaka. Katika kipindi kilichopita niliwahi kupokea malalamiko mengi kutoka kwa vijana kuhusu unyanyasaji kutoka kwa raia hao na wakati fulani kuna wafanyakazi walikuwa wakipigwa, nilivalia njuga likaisha.
“Kipindi kilichopita baadhi ya vijana katika kiwanda kimojawapo walikuwa wakinyanyaswa kwa kupigwa, nilipeleka malalamiko kwa sababu niliona walikuwa wakivunja sheria na tumewahi kuwasilisha ripoti katika mamlaka za juu kuhusu matatizo yao lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa,” amesema.
Mariam Lukindo, aliyewahi kufanya kazi katika kiwanda kimoja wapo anabainisha kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa vifaa vya kujilinda na mikataba halali katika viwanda, kwa sababu wanapewa mikataba isiyo na msingi ili waweze kuendelea na kazi lakini likitokea tatizo hawapati msaada.
“Kwa bahati, niliwahi kupata nafasi ya kufanya kazi katika moja ya viwanda hivyo, hali ni mbaya kwa upande wa mikataba na hakuna vifaa vya kujikinga dhidi ya hatari,” amesema.
Mbali ya vifaa vya usalama, amesema muda wa mapumziko ya chakula ni mfupi na wanafanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.
“Katika kipindi hicho nilikuwa nikilipwa kati ya Sh 6,000 hadi Sh 65,000. Pia kuna mikataba ya muda lakini haitekelezwi ipasavyo, kwa sababu kile kilichoandikwa hakikidhi kile unachopata kila mwezi.
“Mishahara ni midogo na ikiwa utaugua binafsi hakuna matibabu labda ukatike viungo au kiungo na ikiwa utapata ujauzito, basi ni tiketi ya kwaheri hata kama Mchina anahusika,” amesema.
Katibu wa Maendeleo ya Jamii wa Kijiji cha Dundani, Mwenesano Mangosongo, amesema asilimia kubwa ya wafanyakazi katika kata yake wanakabiliwa na changamoto za mikataba na malipo kidogo.
“Baadhi ya wafanyakazi wanakumbana na changamoto ya kilichoandikwa kwenye mikataba ni tofauti na wanachopata, mfano wanapokea Sh 6,000 lakini wanapofanya kazi wanapata Sh 4,000 kila siku.
“Hawa watu wanalazimika kufanya kazi kwa sababu ya umaskini kwa malipo ya chini ya kiwango. Hali hii inawafanya kuingia katika ajira zisizofaa na kufanya kazi hatarishi bila vifaa ili wapate riziki. Hali hii si sahihi, na ndiyo maana tumeshuhudia vijana wengi wakipata matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na kupoteza viungo,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja Rasilimali Watu wa Kiwanda cha Uni Fly, Dennis Mwanyelo, amekiri kuwapo changamoto hizo kwa baadhi ya wafanyakazi kukosa mikataba lakini amedai ni uzembe wao, kwa sababu wakipewa hawaitaki kisha wanaitupa, ndiyo maana wakipata ajali wanawapatia ili wafanikishe mchakato wa ulipwaji wa stahiki zao wakienda Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
“WCF wanawasadia wafanyakazi wakiumia, tunatoa taarifa na akimaliza matibabu tunamwelekeza kwenda kufuata haki yake huko. Sasa kinachotokea hawafuatilii sehemu husika na hawapeleki vielelezo vinavyohitajika ndiyo maana wanakwama,” amesema.