*Ya kupelekwa nje ya nchi yaishia ‘sheli’ za ndani

*TBS wasuasua kutekeleza masharti ya mkataba

Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wimbi jipya la uhujumu uchumi kupitia biashara ya mafuta yanayosafirishwa kwenda mataifa jirani limeibuka, huku mamlaka za serikali zikihusishwa na mwenendo huo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa maelfu ya lita za petroli na dizeli, ambazo zinapaswa kufika katika mataifa hayo kupitia bandari za Tanzania, zinaishia kuuzwa kwenye soko la ndani kinyume cha sheria.

Gazeti hili limepokea orodha ya kampuni za mafuta zinazodaiwa kujihusisha na uchepushaji huo. Hata hivyo, taarifa kamili itachapishwa baada ya kuzungumza na wahusika wote ili kupata mtazamo wao juu ya tuhuma hizi.

Chanzo kikuu kinachotajwa kuchochea hali hii ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambalo mwaka 2021 lilikabidhiwa dhima ya kuweka vinasaba kwenye mafuta, baada ya kampuni ya Global Fluid International (GFI) kupokwa zabuni siku chache kabla ya muda wake kuisha Aprili 2021.

TBS wanatuhumiwa kufeli kutekeleza matakwa ya kimkataba ambayo pamoja na mambo mengine, yalitaka shirika hilo liipatie EWURA ving’amuzi 11 (magari maalumu yenye mitambo ya kisasa kwa ajili ya kupima vinasaba kwenye mafuta). Mwaka mmoja uliopita bei ya kila king’amuzi ilikuwa wastani wa Sh milioni 150.

TBS inasema tayari imekabidhi ving’amuzi hivyo EWURA, ingawa uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kipengele hicho muhimu kwenye mkataba hakijatekelezwa, na kwamba upimaji mafuta ni kaa haupo.

Kwa mujibu wa mkataba, ving’amuzi 11 vilitakiwa kukabidhiwa EWURA. Mchanganuo wa ving’amuzi ulivyo ni kama ifuatavyo: Ving’amuzi 3 vya kutembea kwa ajili ya kuhakiki vinasaba kwenye maeneo mbalimbali ya kuuzia, kusafirisha, na kuhifadhi. Hivi TBS wanasema vimekabidhiwa vyote, ingawa uchunguzi umebaini kuwa havipo.

Mkataba ulitaka vifungwe ving’amuzi 6 kwa ajili ya upimaji wa hiari katika maeneo ya Tanga, Mtwara, Dar es Salaam, Iringa, Tabora, na Chalinze. Katika idadi hii, ni vituo vitatu tu vimekabidhiwa ving’amuzi katika maeneo ya Korogwe – Tanga, Nzega – Tabora, na Igumbilo – Iringa.

TBS wanakiri kuwa ving’amuzi vingine 3 havijafungwa katika maeneo ya Chalinze, Kongowe – Dar es Salaam, na Mtwara kwa madai kwamba bado wanatathmini utendaji kazi wa maeneo yaliyofungwa ving’amuzi kwa upimaji wa hiari. Wanatoa sababu ya kutofunga kwamba wadau wamekuwa hawajitokezi kutumia vituo vilivyokwishanzishwa.

TBS wanadai kuiwa king’amuzi kimoja kwa ajili ya ufuatiliaji wa ubora wa vinasaba, na kingine kimoja kwa ajili ya dharura kimekabidhiwa.

Wakati TBS wakisema hivyo, uchunguzi umebaini kuwa hadi sasa EWURA wana king’amuzi kimoja tu kinachofanya kazi, ambacho kipo tangu zama za GFI. Ving’amuzi vingine ni vibovu.

“Kwa maana hii upimaji vinasaba kubaini mafuta ya dumping haufanyiki kwa sababu TBS hawajatekeleza mkataba wa kununua ving’amuzi na kuvikabidhi EWURA,” kimesema chanzo chetu.

Soko la ndani la mafuta hapa nchini, kwa mujibu wa TBS ni lita mlioni 12 kwa siku; ambazo ni sawa na lita bilioni 4.32. Mafuta haya yanapaswa kuwekwa vinasaba kwa Sh 7 kwa kila lita moja. Hii ina maana kwamba kama TBS wataweka vinasaba kwenye mafuta hayo yote, watavuna Sh bilioni 30.24 kwa mwaka.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa mafuta yanayosafirishwa nje ya nchi bila kulipiwa kodi, na ambayo baadhi yanachepushwa na kuuzwa hapa nchini ni lita bilioni 4.9 kwa mwaka.

Dosari nyingine ni TBS kuendelea kutumia mfumo wa kutumia mikono (manual) katika kupima na kuweka vinasaba; hatua ambayo inaambatana na makosa ya kibinadamu. Kwenye mkataba walitakiwa wafunge mifumo ya semi-automation, au full automation.

Wanajitetea kwa kusema, “TBS inatumia mfumo wa semi-automation katika kupima vinasaba. Hadi sasa kati ya maghala 22, maghala 19 yamefungwa mfumo wa semi-automation.”

TBS wanakiri walau kwa idadi ndogo ya namba kuwa kwenye maghala mengine bado kuna mwanya huo wa kupima kwa kutumia mikono.

“Maghala 3 yaliyobaki, yaani Oil Com – Dar es Salaam, Sahara, na Malawi Cargo Company Ltd (MCC), bado hayajafunga mfumo huu kutokana na vyumba vya kupimia vinasaba kuwa vidogo kupokea mfumo wa semi-automation.

“Mfumo utafungwa pindi wenye maghala watakapokamilisha ujenzi wa vyumba hivyo, kama walivyoahidi kutoa vyumba stahiki vya kupokea mfumo,” imesema taarifa ya TBS kwa JAMHURI.

Kuhusu usalama wa vinasaba, TBS wanasema wanatumia mifumo ya CCTV Camera. Pia wanatumia mifumo ya kielektroniki kuwasilisha taarifa kwa wadau kwa kuwa mifumo ya semi-automation na uhakiki wa vinasaba kwenye mafuta imeunganishwa moja kwa moja na mifumo ya kielectroniki ya kuwasilisha taarifa kwenye mfumo kuwa wa papo kwa papo

“Hakuna changamoto kubwa zinazotukabili kwenye suala zima la uwekaji vinasaba na shughuli zinaendelea kama kawaida,” wanasema TBS.

Kwa upande wao EWURA, wameliambia JAMHURI kuwa hawahusiki na uwekaji vinasaba kwenye mafuta, na kwamba masuala yote yanayohusu programu hiyo waulizwe TBS.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Mchemba, ametatafutwa azungumzie dosari hii kwenye biashara ya mafuta, lakini hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa katika ofisi yake ambaye hakutaka anukuliwe, amesema kuna tatizo kubwa la usimamizi wa mafuta yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Tatizo lipo, tena kubwa. Kwa upande mmoja lipo TBS maana wameshindwa kutekeleza matakwa ya mkataba. Wameshindwa kuleta ving’amuzi ili kung’amua mafuta ambayo hayana vinasaba ambayo kwa maana hiyo yanasafirishwa kwenda mataifa jirani,” amesema.

Anatoa mfano kuwa mwaka Desemba 2020 hadi Machi 2012 ukaguzi wa vinasaba kwenye mafuta uliofanywa katika vituo 276, vituo 10 vilikutwa vina mafuta yasiyo na vinasaba.

“Kituo kimoja kililipa TRA Sh milioni 32. Haya matukio yalikuwapo wakati wafanyabiashara wakijua ukaguzi unafanywa, sasa kwa kukosekana ving’amuzi hali itakuwa mbaya zaidi,” amesema ofisa huyo.

Taarifa ya utendaji kazi ya EWURA inaonyesha kuwa Kati ya Julai na Desemba, 2021 vituo vilikaguliwa na 65 507 (asilimia 12.82) kati ya hivyo vilikutwa vina mafuta yasiyo na vinasaba.

Februari 2023 kulifanyika ukaguzi wa sampuni 155 kwenye malori 32 yanayosafirisha mafuta kutoka kwenye maghala jijini Dar es Salaam. Baada ya kukaguliwa, malori mawili yalibainika kuwa na shehena ya mafuta yaliyowekwa vinasaba vingi Zaidi kinyume cha Kanuni Na. 4(2) na Kanuni Na.6 (2) ya Uwekaji Vinasaba kwenye Mafuta.

Hali hiyo, ilielezwa kuwa ni kiashiria tosha kwamba kuna hujuma na utiaji shaka wa mfumo mzima wa ulinzi na uwekaji vinasaba kwenye mafuta.

Pia kumekuwapo tofauti ya matokeo kwenye vipimo vinavyopimwa kwa sampuli ile ile kwa siki tofauti. Hali hiyo, inatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na baadhi ya wafanyabiashara kwani vipimo vya TBS husoma na kutoa matokeo tofauti kwa siku tofauti kwa bidhaa ile ile moja.

Shaka nyingine iliyopo ni kuwa usalama wa vinasaba namna vinavyohifadhiwa ni jambo linalopaswa kutazamwa upya ili kuhakikisha kuwa haviingii mtaani.

“Uanzishwaji wa petrol stations nyingi kila mtaa, kila mahali ni kiashiria kinachopaswa kuzifanya mamlaka za serikali zianze kujiuliza maswali mengi. Utakuta mafuta haya ya transit yanarudi hapa hapa nchini na hayalipiwi kodi. Hili linawezekana likawa linachangiwa na vinasaba kama vipo mitaani.

“Industrial analysis inaonyesha kuwa bei za mafuta zikishuka wafanyabiashara ya mafuta hulalamika, bei zimekuwa zikishuka kwa miezi minne sasa na wako kimya. Hii ina maana gani? Ina maana kuna dumping,” amesema.

Usuli:

Programu ya Uwekaji Vinasaba kwenye mafuta yanayosambazwa nchini Tanzania ilianzishwa na kusimamiwa na EWURA kuanzia Septemba 2010.

Programu hii ilihusisha mafuta ya petroli, dizeli, na mafuta ya taa yanayotumika nchini, ingawa haikuhusisha mafuta yasiyolipiwa kodi, ambayo ni yale yanayopitishwa kuelekea nchi jirani au yale yanayotumika kwenye miradi maalumu yenye msamaha wa kodi.

Mpango huu ulianzishwa kwa lengo la kudhibiti ubora wa mafuta, kupambana na udanganyifu wa kodi, na kuunda mazingira ya biashara sawa kwa wafanyabiashara wa mafuta. Hii ilifanywa kupitia kanuni maalum za uwekaji vinasaba, maarufu kama The Petroleum (Marking and Quality Control) Rules, 2010.

Kampuni ya kutekeleza programu hii ilichaguliwa kupitia mchakato wa zabuni za kimataifa, ambako sheria na kanuni za ununuzi zilifuatwa kwa umakini. Kampuni ya GFI ilishinda zabuni ya kwanza, na mkataba wake ulianza Septemba 2010 na kumalizika Novemba 30, 2013.

Baada ya kumalizika kwa mkataba wa kwanza, GFI ilishinda zabuni ya pili, ambako mkataba ulianza Desemba 1, 2013, na kumalizika Machi 31, 2017.

Katika zabuni ya tatu, SICPA SA kwa ushirikiano na GFI walishinda, na mkataba wao ulianza Aprili 1, 2017, na kumalizika Machi 31, 2020. Mkataba huu uliongezwa muda mpaka ulipoputwa rasmi Aprili 14, 2021.

Katika mabadiliko yaliyofanyika Aprili 2021, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliondoa jukumu la kuweka vinasaba kwenye mafuta kutoka kwa kampuni binafsi (SICPA SA kwa kushirikiana na GFI) na kukabidhi jukumu hilo kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Serikali ilivunja mkataba huo wiki mbili kabla ya ukomo wake, na kuna habari kwamba kampuni hiyo ilifungua madai ya kulipwa mabilioni ya shilingi.

TBS ilianza rasmi utekelezaji wa kuweka vinasaba kwenye mafuta tarehe 28 Aprili 2021.

Mfumo wa kuweka vinasaba kwenye mafuta kwa kutumia teknolojia ya molecular marker unajumuisha vipengele viwili. Mosi, uwekaji vinasaba kwenye mafuta (dosing) – hutegemea aina ya miundombinu na changamoto zinazokuwapo.

Pili, utambuzi wa vinasaba, ambako kuna njia mbili za utambuzi: moja ni utambuzi wa kuangalia kwa macho (visual inspection), na nyingine ni utambuzi wa kutumia vifaa maalumu vya maabara, kama vile ving’amuzi, kutegemeana na aina ya vinasaba.

Utambuzi kwa macho ni teknolojia dhaifu na hutumika pale ambako uwekaji vinasaba unahusisha matumizi ya rangi.

Teknolojia hii imepitwa na wakati na hutoa mianya ya udanganyifu. Teknolojia inayofaa kwa serikali kukabiliana na wadanganyifu ni ya molecular marker inayotumia vinasaba ambavyo ni kemikali.

Mwanya huu kwenye uwekaji vinasaba unatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazofanya biashara ya mafuta yanayochepushwa ishamiri nchini, huku mtandao huo ukiwahusisha watendaji ndani ya taasisi nyeti za serikali.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa Mamlaka yas Mapato Tanzania (TRA), Kayombo, ameomba taarifa zaidi ili idara inayohusika dhidi ya ukwepaji kodi ichukue hatua.