Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza ujenzi wa barabara ya Kimara – Mavurunza – Bonyokwa hadi Kinyerezi , jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilomita saba kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa na kampuni ya kizawa ya Nyanza Road Works, ambapo barabara hiyo inatarajiwa kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa Ubungo na Segerea jijini humo pindi itakapokamilika.
Ujenzi huo unatarajiwa kupunguza changamoto za miundombinu na usafiri kwa wananchi wa maeneo ya Kimara, Bonyokwa, Kinyerezi, na maeneo jirani.
Pia, wanatarajia kunufaika kiuchumi kupitia fursa zitakazotokana na mradi huu, ikiwemo biashara na huduma nyingine zinazotokana na uboreshwaji miundombinu bora ya barabara.
Ujenzi wa mradi huo unajumuisha daraja kubwa lenye urefu wa mita 25, pamoja na madaraja madogo saba ya kalvati, ambayo yatasaidia kupitisha maji wakati wa mvua kubwa.
Aidha, mradi huo utahusisha ufungaji wa taa za barabarani, hatua inayolenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara hiyo.
Mradi huo unalenga kuimarisha miundombinu ya jiji, kuboresha huduma za usafiri, na kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na viunga vyake.
