*Mapato ya mazao ya uvuvi yaongezeka maradufu ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wavuvi boti za kisasa

Na Joe Beda, JamhuriMedia, Pangani

Ni siku ya Jumatano, Februari 26, 2025 nipo jijini Tanga. Mji umechangamka kwelikweli.

Kisa? Kiongozi mkuu wa nchi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan yupo katika ziara rasmi ya kikazi mkoani Tanga na leo anakwenda wilayani Pangani.

Pangani. Ninapafahamu kwa miaka mingi sana, lakini amini usiamini sijawahi kufika!

Kwetu wapenzi wa historia huwezi kuitaja Pangani pasina kumzungumzia mfanyabiashara; Al Bashir bin Salim al-Harith; almaarufu Abushiri (1833 – Desemba 15, 1889).

Mwamba huyu. Ndio. Huwezi kupanga vita na Wajerumani wa sasa na hata wale wa kale kama wewe si mwamba. Abushiri ni mwamba, na Pangani ndio kwake.

Ninawasili stendi ‘kuu’ ya Pangani saa tatu na nusu asubuhi.

“Huu mji umesahaulika pamoja na ukongwe wake wote!” ninawaza moyoni kwa masikitiko. Pangani niliyokuwa nikiifikiria sio hii niliyoiona.

Rais Sakia Suluhu Hassan akimkabidhi mmoja wa wanufaika cheti cha uvuvi

Nikatamani kuwatafuta ‘wazee wa mji’ nizungumze nao mawili matatu kuhusu Abushiri na kukwama kwa maendeleo ya Pangani, lakini hili silo lililonileta leo.

Kwa kuwa sikuwa ninajua ninakopaswa kuelekea, ninalazimika kuchukua bodaboda.

“Mama anakuja huku leo, vipi, unajisikiaje?” ninamuuliza mwendesha bodaboda aliyekuwa amevalia vazi rasmi kwa ajili ya mapokezi ya Rais Samia, pamoja na kofia iliyoandikwa ‘Jumaa Aweso’.

“Acha kabisa, leo ni siku ya furaha sana kwetu. Kama unavyoona, biashara imeshachanganya asubuhi asubuhi,” ananijibu na kuniuliza: “Tunakwenda wapi mzee?”

Ninamuuliza kama anafahamu sehemu ambako Rais atakuwa ‘akigawa’ boti za kisasa kwa wavuvi wa Pangani na mkoa mzima wa Tanga.

Mara moja akawasha mashine. Mitaa miwili mitatu, tukafika ufukweni; Bandari ya Pangani.

Naam, hapa ndipo patakapofanyika shughuli iliyonileta Tanga. Maneno yaliyoandikwa katika bango la kwanza tu ninaloliona, yananivutia; ‘Uvuvi ni Utajiri’.

“Mh!” ninawaza moyoni huku nikisita kidogo. “Uvuvi ni utajiri au kuna wavuvi matajiri?”

Ninaliona bango jingine kubwa zaidi linalosomeka: ‘Uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Ugawaji wa Boti za Kisasa kwa Wavuvi’. Sasa hii ndio shughuli yenyewe.

Waswahili husema ‘shughuli ni watu’; na hapa ufukweni pana watu wa kutosha.

Ajabu ni kwamba, si ufukweni pekee kwani hata ndani ya maji (baharini) kuna makumi ya watu; vijana.

Hawa walikuwa ndani ya boti nzuri za kisasa zenye rangi nyeupe tayari kumsikiliza Rais Samia.

Pahe Restaurant, mgahawa uliopo ufukweni ndio unanipa hifadhi pamoja  na ‘view’ nzuri kushuhudia yote yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya Rais kuzindua mradi wa ugawaji boti asubuhi hii.

Saa tano kasoro dakika chache, Mama Samia akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Burian, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji na maofisa wengine kadhaa wanawasili eneo la tukio na kuibua shangwe kwa vijana wavuvi waliokuwa baharini na boti zao.

“Nimetoa boti 35 kwa wavuvi wa Mkoa wa Tanga. Na hii ni awamu ya pili. Kila boti ina uwezo wa kubeba kati ya tani tatu hadi tano za samaki.

“Haya ni mavuno makubwa sana. Boti hizi ni imara na zina nguvu kuliko zile za kienyeji (za mbao) na zinafika hadi karibu na bahari kuu,” ninamsikia Dk. Samia akizungumza baada ya kubonyeza kitufe (king’ora) kuashiria kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya ugawaji wa boti za kisasa kwa wavuvi wa maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya wanufaika wa boti za uvuvi wakimsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan

Ninawaza. Kwa miaka mingi wavuvi wamekuwa miongoni mwa makundi yenye mchango mkubwa kwa jamii kiafya na hata kiuchumi. Kiuchumi?

Hapana. Ni kiafya zaidi, kiuchumi sina uhakika. Mara ninakumbuka lile bango ambalo sasa lipo mbele ya Rais Samia; ‘Uvuvi ni Utajiri’.

Ni nani aliyebuni kaulimbiu hii? Je, anataka kusema nini? Ana uhakika kwamba kwenye uvuvi kuna utajiri?

Mawazo yangu yanakatizwa ghafla na sauti ya Waziri Dk. Kijaji akimweleza Rais Samia: “Boti hizi 35 utakazowakabidhi wavuvi wa Tanga leo zina thamani ya Sh bilioni 4.7; fedha ulizotukabidhi sisi ili tusizimamie.”

Hii ikanishitua. Serikali inatoa Sh bilioni 4.7 za walipa kodi ‘kuwapa’ wavuvi? Ni sahihi kweli?

Ninafungua makabrasha yangu kuhakiki usahihi wa ‘figures’ zilizotajwa. Humu nakumbana na maneno haya:

“Awamu ya kwanza ya mradi huu imeanza mwaka wa fedha 2022/2023 na kugharimu Sh bilioni 11.5 ‘kuwakopesha’ wavuvi boti za kisasa na vifaa vyake kwa masharti nafuu.

“Jumla ya boti 160 zimekopeshwa kwa wanufaika 3,163 wanawake kwa wanaume katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa nyasa.”

Kwa hiyo, achilia mbali Sh bilioni 4.7 za hizi boti 35 zilizopo mbele yangu, tayari kuna Sh bilioni 11.5 zimeshakopeshwa kwa wavuvi!

“Awamu ya pili ya mradi imeanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2024/25. Wizara imetenga Sh bilioni 14.4 na tayari Sh bilioni 11.5 zimetolewa kununua boti 120 na vifaa vyake, ikijumusha boti saidizi,” sauti ya Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uvuvi (mvuvi mwandamizi), Profesa Mohamed Sheikh, inasikika.

Hapo ndipo nikahitimisha moyoni na kwa msisitizo kwamba iwapo serikali inaendeelea kutoa fedha zote hizi… “It means thisi is real business.”

Profesa Sheikh anaendelea: “Zaidi ya ajira 5,000 zimepatikana tangu mradi huo ulipoanza mwaka jana.

“Tangu kuanza kugawa boti hizi, uzalishaji wa samaki nchini umeongezeka kwa takriban mara mbili.

“Pia thamani ya usafirisha wa mazao ya uvuvi nje ya nchi nayo imeongezeka kutoka Sh bilioni 447 hadi kufikia Sh bilioni 558.

“Haya ni mfanikio yaliyochagizwa na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia mikopo nafuu isiyokuwa na riba. Riba yake ni asilimia sifuri.”

Hapo moyo ukatulia. Kumbe huu ni ‘uwekezaji’ kwa wavuvi na si ‘ugawaji’ (boti) kwa wavuvi. Serikali imewekeza. Afadhali.

Hafla inakwisha, Rais anaondoka. Anakwenda uwanjani kuzungumza na wananchi. Mimi bado nina hamu ya kufahamu mengi zaidi.

Nyumba ya kisasa iliyopo Kijiji cha Zingibari, Mkinga mkoani Tanga iliyojengwa kutokana na mikopo inayotolewa na serikali kwa makundi maalumu.

Nakutana na Sitaruka Njama Bwago, mmoja wa wanufaika wa uwezeshaji (si ugawaji) wa boti za kisasa, ambaye anakiri kuwa ‘uvuvi ni utajiri’.

“Kinachofanywa na Rais Samia ni jambo kubwa linalostahili kupongezwa na kila mtu anayependa maendeleo kwa sababu hili linazigusa familia nyonge kabisa,” anasema Bwago, mmoja kati ya wanufaika binafsi ilhali wengine walikuwa ni wa vikundi.

Anasema kwa kuwa boti moja hutoa ajira kwa watu 30, maana yake kwa boti 35 zilizotolewa Pangani maelfu ya watu watanufaika.

“Miaka michache ijayo uchumi wa wavuvi wa ukanda wa pwani hususan huku kwetu Tanga, utabadilika na kuwa bora zaidi kutokana na utashi wa kiongozi wetu mkuu, Rais Samia, wa kuwagusa hata watu wa familia duni na nyonge kama hizi za kwetu,” anasema.

Bwago anamtaja Amina Mwantumu Msuke kama mfano wa wanufaika ambaye baada ya kupata boti moja awamu ya kwanza, amefanikiwa kuongeza boti nyingine kwa fedha za faida huku akiwa mlipaji mzuri wa deni la serikali.

Ninakutana na Profesa Sheikh pamoja na wasaidizi wake kadhaa. Ninashindwa kuyanasa majina yaomara moja ila la mmoja tu, Katunzi.

Wote wanaonyesha furaha waliyokuwa nayo baada ya kukamilika shughuli ya uwezeshaji wa wavuvi.

“Tumejifunza mengi sana na sasa kazi hii imekuwa rahisi kuliko ilivyokuwa mara ya kwanza. Yaani Rais anaondoka, na bot izote zinaondoka kwenda kuanza maandalizi ya kuongia baharini,” anasema ofisa mmoja wa Idara ya Uvuvi.

Kutoka kwa Profesa Sheikh ninatamani kujua iwapo mazao ya uvuvi yanaongezeka, wamejiandaa vipi katika kutafuta masoko?

“Hatuna shaka na soko la mazao ya uvuvi la ndani au la nje ya nchi. Masoko ya nje ya nchi yapo ya kutosha.

“Tanzania kuna viwanda 64 vya kuchakata samaki; viwanda 12 kati ya hivyo hupeleka bidhaa zake kwenye masoko ya Ulaya.

“Na mazao (ya uvuvi) hayatoshi. Kwa hiyo uwekezaji huu utaendeleza shughuli za uvuvi na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.”

Ni kutokana na kukua kwa kipato cha mtu (mvuvi) mmoja mmoja ndio maana Profesa Sheikh anaamini kuwa; ‘uvuvi ni utajiri’.